Vikwazo saba vinavyowakwamisha Watanzania kuwekeza

Mwanza. Ukosefu wa mitaji, elimu, ardhi, uwoga, kodi kubwa ya uingizaji vifaa kutoka nje ya nchi, ukosefu wa mbinu, na uwepo wa dhana potofu kuwa wawekezaji ni lazima watoke nje ya nchi, ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakwamisha wazawa kuwekeza nchini.

Sababu hizo zimetajwa leo Julai 18, 2024 na Mkurugenzi na Mmiliki wa Kiwanda cha Joasamwe Investment, Kapocha Masatu alipokuwa akizungumza na Kamati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) iliyotembelea kiwanda hicho kilichopo Nyakato katika Manispaa ya Ilemela mkoani hapa.

Amesema kama changamoto hizo zitatatuliwa, zitachochea uwekezaji kwa Watanzania.

“Watanzania wengine wanashindwa kuwekeza kwa sababu ya uoga. Wengi hawana uthubutu wa kwenda kuangalia fursa nje ya nchi na kuzileta nyumbani. Sasa tukisema tuwaachie watu kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza wakati na sisi tunao uwezo huo inakuwa siyo vizuri. Kwa hiyo niwaombe vijana tutoe uoga,” amesema.

Masatu amesema Serikali inapaswa kuboresha eneo la kodi ya vifaa vya kutoka nje; “Ukiangalia kwetu ni changamoto sana kwa sababu tunalipia asilimia 25 ya thamani ya hivyo vifaa ukizingatia kama ndo unaanza, inakuwa ngumu,” amesema Masatu.

Meneja Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe amesema ukosefu wa mitaji na mbinu za kuwezesha viwanda vidogo kukua ikiwemo namna ya kupata changamoto inapelekea Watanzania kushindwa kuwekeza.

“Changamoto moja kubwa ni uthubutu kwa sababu unaweza kuwa na mtaji lakini ukashindwa kuthubutu kuwekeza lakini pia  ukosefu wa mbinu mbalimbali za kuwezesha viwanda vidogo viweze kukua ikiwemo namna ya kupata teknolojia pia ni sababu, nafikiri tukitoa elimu kwa watu na mitaji ikatolewa wengi watahamasika kuwekeza,” amesema Songwe.

Kwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TIC, Pascal Maganga ametaja ukosefu wa elimu, kodi kubwa ya uingizaji vifaa nchini na ardhi ni sababu ambazo hutajwa na watanzania wengi kuwa zimesababisha washindwe kuwekeza nchini.

“Changamoto ambazo tunazisikia kutoka kwa wawekezaji ambazo zimebakia na sisi tunapambana nazo kutatua mfano kwenye kiwanda hiki amelalamikia msamaha wa kodi ya uingizaji magari nchini hakupa lakini sababu ilikuwa kwa sababu hakuwa na elimu, lakini changamoto nyingine ni ardhi mfano huyu amesema ana eneo dogo kwa hiyo angepata eneo kubwa angeweza kutanua mradi wake,” amesema.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Maganga amesema TIC inaendelea kutoa elimu kwa wawekezaji wa Kitanzania, wafanyabiashara, wajasiriamali, na wananchi wengine ili kuwavutia zaidi kuwekeza katika sekta mbalimbali.

“Sisi kama TIC tupo hapa kwa ajili ya kutoa elimu na kuendesha zoezi la kujisajili kwa wadau ambao ni wawekezaji lakini, pia hata kesho Julai 19, 2024 tutafanya semina kubwa kwa wadau kama wafanyabiashara, waandishi wa habari na makundi yoyote waje watusikilize ili tutoe ile elimu ya uwekezaji na taratibu za kujiunga na kituo cha uwekezaji ili waweze kupata faida,” amesema Maganga.

Related Posts