Mauya aukubali mziki wa Singida BS

KIUNGO mkabaji wa Singida Black Stars, Zawadi Mauya  amesema kwa usajili uliofanywa na timu hiyo, anaamini ushindani utakuwa mgumu kuanzia kwa wachezaji wenyewe hadi timu pinzani.

Mauya amejiunga na timu hiyo, akitokea Yanga ambayo aliitumikia kwa misimu minne, alisema maisha ya soka ni popote, kikubwa anajipanga kuhakikisha anakuwa msaada katika majukumu yake mapya.

“Utofauti ni ukubwa wa jina la Yanga, ila kwa wachezaji waliopo Singida Black Stars, wazuri na nauona ushindani utakavyokuwa mkubwa katika mechi za mashindano mbalimbali,” alisema.

Pia alizungumzia kukutana na mshambuliaji Joseph Guede ambaye alicheza naye Yanga kwa muda mfupi, anakiri ni mchezaji mzuri anaona ataisaidia timu hiyo.

“Jamaa ni mpambanaji, anazungumza na kila mtu, japokuwa nimefanya naye kazi Yanga kwa kipindi kifupi, lakini naamini tutafanya kazi nzuri kwa pamoja tukiwa hapa,” alisema.

Mauya hakutaka kumsahau mshikaji wake, Bakari Mwanyeto ambaye ni nahodha wa Yanga, kwamba licha ya kukaa kwa pamoja, lakini wamefanya vitu vingi vikubwa.

“Wakati naondoka Yanga, Bakari alikuwa wa kwanza kufahamu hilo, alinitakia kila la kheri ya mapambano mapya, ingawa maisha ya mpira ni yale yale, huenda tutakutana pengine, kama nilivyokutana na washikaji wengine katika timu ya sasa,” alisema.

Related Posts