WANACHAMA wa Simba Mkoa wa Mwanza wameanza mapema kujipanga kwa safari ya kwenda jijini Dar es Salaam kuiunga mkono timu yao katika tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 3, mwaka huu.
Katika kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri, viongozi wa klabu hiyo mkoani hapa kwa nyakati tofauti walikutana na viongozi wa matawi mwishoni mwa wiki iliyopita na Jumatatu kujadili mipango ya safari hiyo na namna watakavyoisherehekea siku hiyo.
Katibu wa Simba Mkoa wa Mwanza, Philbert Kabago alisema Simba Day ni sikukuu hivyo wanajipanga kuifurahia kwa namna ya kipekee na wanachama na mashabiki wanaohitaji kwenda Dar es Salaam kushuhudia tukio hilo watagharimia Sh100,000, huku wakitarajia kuondoka jijini hapa kuanzia Julai 29.
“Tumejipanga vizuri na Simba Day kutoa misaada, kuchangia damu na kufanya usafi na safari ya kwenda jijini Dar es Salaam, yapo pia matawi yameratibu usafiri wao binafsi. Simba Day ni kama sikukuu tumeambiwa kuna matawi yameshanunua ng’ombe, mbuzi na mchele kusherehekea siku hii,” alisema Kabago.
Mwanachama wa timu hiyo, Jamila Juma alisema tawi lake wameshanunua ng’ombe na mchele kunogesha siku hiyo na kuchangia damu, huku Mariam Shaban akitamba kwa usajili wa timu yake msimu huu.
“Tunaamini Simba ya sasa ni Simba mpya ya moto, naamini hatutarudi tulikotoka kwa sababu tumesajili vizuri, viongozi wamekuwa wamoja kwa hiyo hatuna kikwazo tena,” alisema Mariam.
Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo mkoani hapa, Omary Makoye alisema msimu huu utakuwa na matumaini kwani viongozi wamejitahidi kurekebisha makosa na kufanya usajili mzuri.