Dk Mataragio aagiza kituo kujaza gesi Dar kukamilika Desemba

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amemwagiza mkandarasi wa ujenzi wa kituo mama cha kujaza gesi asilia kwenye magari eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kukamilisha mradi huo kufikia Desemba mwaka huu.

Mkandarasi wa kituo hicho ni Sinoma International Engineering Co. Ltd ya nchini China.

Kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kushindilia gesi yenye ujazo wa futi milioni tatu kwa siku na kitahudumia magari na viwanda kikiwemo kiwanda cha dawa Kairuki kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Dk Mataragio ameyatoa maagizo hayo leo Julai 18, 2024 baada ya kutembea mradi huo unaotekelezwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Hii ni sehemu ya mikakati ya nchi ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza tutumie nishati safi, kwa hiyo kupitia mradi huu maeneo yote ambayo hatuna miradi ya gesi tutatumia kituo hiki kusafirisha gesi kupitia magari kutoa huduma hiyo ndio maana nimeagiza mradi huu ukamilika kabla ya Desemba,” amesema.

Dk Mataragio amesema kituo kinachojengwa Chuo KIkuu cha Dar es Salaam kitahudumia magari na vituo vya kujaza gesi asilia akisisitiza kuwa uwekezaji katika sekta ya gesi utaendelea kuongezeka.

Mkurugenzi wa mkondo wa chini wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emanuel Gilbert amesema kituo hicho kitakapokamilika wakazi wa Morogoro, Mbeya na Tanga watapata gesi asilia.

Njia itakayowezesha upatikanaji huo ni kupitia magari maalumu ya kusafirisha gesi iliyoshindiliwa.

 “Pamoja na kuwa na eneo la kutoa huduma ya gesi kwa magari yanayopatikana Dar es Salaam yapo magari yatanunuliwa ikiwa ni sehemu ya huu mradi ambayo yatapeleka huduma ya gesi kwa wateja watakaohitaji.

“Baada ya mwezi wa 12 mtu aliyepo mkoani ataweza kuanzisha kituo chake cha gesi na kuja kuingia makubaliano na sisi tukawa tunampatia huduma ya gesi,” amesema.

Tanzania inakadiriwa kuwa na mita trilioni 230 za ujazo za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.

Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa mkoani Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.

Ripoti ya Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Tanzania 2016-2045 inaonyesha futi za ujazo trilioni 8.8 za gesi zimetengwa kwenye umeme, futi za ujazo bilioni 500 kwenye kaya, futi za ujazo trilioni 3.6 kwenye viwanda na futi za ujazo bilioni 600 kwa magari.

Kwa upande wa gesi kwenye magari, mpaka sasa vituo vinavyotumika kujaza gesi kwenye magari ni kituo mama cha Ubungo kinachohudumia zaidi ya magari 800 kwa siku, Tazara chini ya Kampuni ya Enric Gas Technology Tanzania Limited kikihudumia magari 300 kwa siku na kituo cha Uwanja wa Ndege kinachohudumia magari 1,200 kwa siku.

Mpaka sasa TPDC inashirikiana na sekta binafsi kujenga vituo 30 vya kujaza gesi katika Jiji la Dar es salaam, maeneo vitakapojengwa vituo hivyo  ni maeneo ya Muhimbili, Kibaha, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Sinza, Mwenge, Goba, Mbezi Beach na Mbagala.

Vilevile, TPDC inatarajia kuleta magari ya kujaza gesi kwenye vituo kwa kutumia magari maalum ya kubeba gesi asilia.

Related Posts