Mwanza. Mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19, maradhi, na mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto zinazotajwa na Serikali kuwa zimekwamisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 kwa ufanisi.
Hata hivyo, Serikali imeanza kukusanya maoni kwa umma kuhusiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2050 ili kuhakikisha inakuwa na mpango jumuishi utakaohakikisha hakuna kukwama katika utekelezaji wake hata kama kutatokea janga ama dharura.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Julai 18, 2024, na Mjumbe wa Tume ya Mipango, Balozi Dk Asha Migiro, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusiana na uzinduzi wa kongamano la kwanza la kikanda kuhusu maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 litakalofanyika Jumamosi Julai 20, mwaka huu mkoani hapa.
Dk Migiro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Kitaalamu ya Dira ya Taifa 2050, amesema Serikali itatumia changamoto hizo hususan mvua za El-Nino, tope la Hanang na mafuriko yaliyotokea kama funzo wakati wa utengenezaji wa Dira ya 2050.
“Tunaelewa vizuri jinsi mafuriko yalivyoharibu miundombinu katika vipindi tofauti, hali iliyorudisha nyuma jitihada za Serikali za kujenga miundombinu. Pia, mlipuko wa magonjwa umesababisha mifumo ya afya kuelemewa, kama tulivyoshuhudia hivi karibuni na athari za ndani na nje za Uviko-19,” amesema Dk Migiro.
Amesema hali hiyo ilisababisha rasilimali fedha na watu ambazo zingetumika kutekeleza Dira ya 2025, kuelekezwa kwenye dharura zilizojitokeza. Hivyo, amesema katika maandalizi ya Dira ya 2050, Serikali itajielekeza katika kuzingatia mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kuhusu utekelezaji wa Dira 2025 kikanda, Dk Migiro amesema Tanzania inafanya vizuri kwa kile alichodai ni utekelezaji wa Sera mbalimbali na ufikishwaji wa huduma za msingi kwa umma zikiwamo elimu na afya jambo linalowavuta mataifa mengine kutembelea nchini na kujifunza kupitia mafanikio hayo.
“Tuko Mwanza kuonana na wananchi, viongozi na taasisi kutoa hamasa kwao kushiriki kutoa maoni kuhusiana na Dira ya 2050. Tuna wajibu wa kujipima kujua nini tumekifanya kwenye Dira 2025, tumekwama wapi na tunatakiwa kuelekea wapi kwenye Dira 2050 ili kuleta ustawi kwa Umma,” amesema.
Awali, Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amesema kongamano hilo litakalofanyika Jumamosi Julai 20, 2024, ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa Desemba 9, 2023, ya kutaka kufanyika ukusanyaji wa maoni ya wananchi hususan vijana ili kujenga Dira ya Tanzania yenye uhalisia.
“Dira inachukua mtazamo wa aina ya maendeleo ambayo Watanzania tunayataka ifikapo 2050. Tunawaomba wananchi hasa vijana waje watoe mawazo na michango yao ili itakapofika mwaka 2050 wajue kabisa dira hiyo ni ya kwao. Mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko,” amesema Makoba.
Kwa upande wake Mkazi wa Mkuyuni jijini Mwanza, Fatma Yusuph ameshauri itungwe sheria au sera itakayosimamia utekelezaji wa Dira ya 2050 ili kuhakikisha kunakuwa na usimamizi na uendelevu wa malengo ya nchi hata kama mfumo wa uongozi utabadilika.
“Inatakiwa iwekwe misingi mizuri ili kulinda dira ya nchi. Lazima tutafute mfumo ambao unaweka mwelekeo kiongozi yoyote anayekuja kuufuata, ikibidi itungwe sheria ya kulinda dira,” amesema Fatma.
Dira ya Maendeleo ya Tanzania inayofikia tamati Julai 2025, iliundwa Julai 1999 huku utekelezaji wake ukitajwa kufanyika kwa mafanikio (bila kutaja asilimia), hata hivyo, kuna changamoto zinazotajwa kutakiwa kuongezewa umakini katika utengenezaji wa Dira ya 2050 ikiwemo uwepo wa Akili Mnemba (AI) na athari zake katika mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na ajira.