Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu Mkazi wa Gerezani, Samweli Gombo kifungo cha miaka mitamo jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa fedha kiasi Sh102.9 milioni.
Fedha hizi alizoiba kwenye akaunti ya benki ya NMB ya marehemu baba yake wa kambo, Staniford Gombo.
Pia, Mahakama hiyo imemuamuru mshitakiwa huyo kumlipa mlalamikaji wa kesi hiyo, Yared Gombo ambaye alikuwa msimamizi wa mirathi fidia ya kiasi cha Sh102.9 milioni anachodaiwa kuiba.
Mshtakiwa huyo alikuwa anakabiliwa na mashtaka manne yakiwemo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na wizi wa Sh102.9 milioni.
Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo akisoma hukumu hiyo leo Alhamisi Julai 18, 2024 amesema katika kesi hiyo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shitaka moja la wizi na mashitaka mengine hayakuthibitishwa.
Swalo amesema hakuna ubishi mshitakiwa alitoa fedha katika akaunti ya marehemu, ambapo katika ushahidi wake mshitakiwa huyo alidai fedha hizo alipewa na marehemu (enzi za uhai wake) kupitia wosia aliouacha.
“Kesi hiyo adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano kwa kuwa mshtakiwa amekaa mahabusu mwaka mmoja hivyo atatumikia kifungo cha miaka minne gerezani,” amesema Swalo.
Amesema katika utetezi wa mshtakiwa huyo alishindwa kuwasilisha mahakamani wosia kuthibitisha alipewa fedha hizo wala kumuita mahakamani wakili Dikson Matata anayedai ndiye alishuhudia uandishi wosia huo kuja kuthibitisha hilo.
Amesema wakili Dickson aliyekuwa akitunza wosia huo angetafutwa ili kuthibitisha mahakamani hapo fedha alizopewa mshtakiwa huyo ameshindwa kuthibitisha hilo na ilikuwa ni lazima wosia uwepo ili uwekwe wazi kila mtu auone.
“Kutumia fedha za marehemu kwa madai kwamba kulikuwa na wosia ni kosa kisheria, hakuwa na mamlaka yoyote ya kutumia fedha za marehemu, hakuwa na dai lolote la haki na amewadhurumu wale wote waliokuwa wana haki,” amesema Swalo.
Kutokana na hayo mahakama hiyo imethibitisha kosa hilo hivyo mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka mitano ikihesabika na mwaka mmoja aliokuwa amekaa mahabusu
Inadaiwa Stanford Gombo aliyekuwa baba wa mshitakiwa Samwel, alifariki dunia Novemba 11, 2017 na kuzikwa Novemba 13 mwaka huo ambapo aliacha mali mbalimbali ikiwemo Sh102.9 milioni alizoacha katika Benki ya NMB.
Ilidaiwa mwaka 2019 familia ya Stanford ilikaa kikao cha familia na kumteua Yared Gombo kuwa msimamizi wa mirathi.
Kwamba mshitakiwa Samwel alibaki na kadi ya Stanford na hakutaka kusema kama anayo licha ya wanafamilia kuitafuta.
Ilidaiwa kati ya Novemba 13, 2017 hadi Juni 30,2018 jijini Dar es Salaam, Samwel alichukua fedha hizo benki katika akaunti ya baba yake.
Iliendelea kudaiwa mshitakiwa huyo aligushi muhtasari wa kikao cha familia, cheti cha kifo cha baba yake akionesha kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na nguvu ya kisheria na kuiwasilisha mahakama ya mwanzo Chakwale, Wilaya ya Gailo mkoani Morogoro.
Kwamba Mei 6, 2022, mshtakiwa huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na makosa hayo.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917