Dar es Salaam. Tanzania imeingia makubaliano na Taasisi ya Bioventure for Global Health (BVGH) ya nchini Marekani itakayosaidia kutoa mafunzo kwa wataalamu wa tiba mionzi ikiwemo upatikanaji wa dawa kwa gharama nafuu.
Mradi utatoa fursa kwa ajili ya tafiti katika huduma za saratani, kuimarisha miundombinu na kuwezesha upatikanaji wa dawa za saratani kwa gharama nafuu kwa Watanzania.
Hatua hiyo inakuja siku mbili, tangu Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Biden Cancer Moonshot ya nchini Marekani, kukaa kikao cha pamoja Ikulu ya Marekani, kutathmini maeneo muhimu ya kushirikiana kupambana na ugonjwa wa saratani nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa jana Julai 17, 2024 katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Washington DC nchini Marekani na kushuhudiwa na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dk Elsie Sia Kanza.
Ushirikiano huo kati ya Wizara ya Afya na taasisi hiyo, unalenga kuimarisha huduma kwa kutoa fursa za mafunzo kwa watalaamu wa saratani wakiwemo madaktari bingwa na wabobezi katika huduma za mionzi.
Akizungumza baada ya kusainiwa makubaliano hayo, Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha huduma za saratani na kuhakikisha zinapatikana kwa urahisi kwa Watanzania ili kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
“Mradi huu pia utatoa fursa kwa ajili ya tafiti katika huduma za saratani, kuimarisha miundombinu ya huduma hizi zote na kuwezesha upatikanaji wa dawa za saratani kwa gharama nafuu kwa Watanzania,” amesema Waziri Ummy.
Mkurugenzi wa Taasisi ya BVGH, Jennifer Bent baada ya kusaini makubaliano hayo ameelezea kufurahishwa kwake na utayari wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na taasisi hiyo pamoja na namna ambavyo serikali imedhamiria kukabiliana na ugonjwa wa saratani.
Makubaliano yaliyofanywa kati ya Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Biden Cancer Moonshot ya nchini Marekani Julai 15, 2024 yalilenga kukabiliana na uhaba wa wataalamu, ukosefu wa miundombinu wezeshi, vifaa tiba hususani vya kutoa huduma za mionzi, takwimu, tafiti pamoja na ubunifu ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora za saratani bila kikwazo.
Kikao hicho kiliandaliwa na Ikulu ya Marekani kupitia Taasisi ya Biden Cancer Moonshot.
Hatua hiyo inakuja wiki chache tangu ripoti maalumu iliyochapishwa na gazeti hili kuhusu changamoto za huduma za tiba za mionzi, ugunduzi wa mapema na changamoto za gharama za matibabu ikiwemo dawa, vipimo na tiba kemikali.
Ripoti hiyo iliyochapishwa kuanzia Juni 24, ilibainisha kuwa wagonjwa wote wa saratani Tanzania wanaolazimika kupata tiba-mionzi, wanategemea mashine tatu pekee.
Mashine hizo, moja ipo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, mkoani Mwanza na mbili zipo Taasisi ya Saratani Ocean Road (Orci) jijini Dar es Salaam.
Kutokana na uchache wa mashine hizo, kumekuwa na foleni ya wagonjwa wanaosubiri kupatiwa huduma.
Uchunguzi huo wa Mwananchi uliofanywa kwa takribani miezi mitatu ulibaini wagonjwa wengi kutopata tiba stahiki kwa wakati kutokana na upungufu wa mashine hizo unaosababisha na kusubiri muda mrefu kufikiwa kwa zamu zao za kupatiwa matibabu. Hali hiyo pia inaweka hatarini maisha yao.
Kwa mujibu wa viwango vya tiba vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) nchi inahitaji kuwa na mashine moja katika kila watu milioni moja, lakini kwa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 60 kuna mashine tatu pekee, hivyo kuwa na uhitaji wa mashine 57 zaidi.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917