Sumaye: Tumuenzi Mandela kwa vitendo

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela wanajamii wametakiwa kumuenzi kiongozi huyo kwa vitendo.

Maadhimisho hayo ambayo hufanyika Julai 18 ya kila mwaka siku ya kuzaliwa ya Mandela kama sehemu ya kutambua mchango wake kwa jamii za Afrika ya Kusini, Afrika na dunia kwa ujumla.

Akizungumza leo Julai 18, 2024 katika hafla maalumu ya kuadhimisha siku hiyo iliyoandaliwa na taasisi ya Victorious Center for Exellence, Waziri Mkuu msataafu, Frederick Sumaye amesema maisha ya Mandela alikuwa kiongozi mzalendo ambaye maisha yake yameacha alama ambayo kila mtu anapaswa kujifunza.

Sumaye amesema Mandela alikuwa kiongozi ambaye alikuwa muumini wa demokarisia, usawa,  haki na usawa, umoja na ushirikiano pamoja na upendo.

Ametoa mfano baada ya Mandela kutoka jela na kushinda uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini na hivyo kuwa rais mpya wa nchi hiyo watu wengi walitarajia angelipiza kisasi kwa makaburu kwa kuwafanyia vitendo vya ubaguzi wa rangi.

“Mandela hakufanya hivyo ila alihimiza umoja, upendo na demokrasia huku akisisitiza haki sawa kwa watu wa rangi zote katika nchi ya Afrika Kusini,” amesema.

Pia, ameongeza kuwa Mandela alikuwa kiongozi ambaye alihimiza umoja na ushirikiano na alikuwa tayari kujitolea kuwasaidia wengine.

“Maisha ya Mandela yametufundisha na ametuachia mambo mengi, kubwa likiwa ni kusamehe na kuwa tayari kujitolea maisha kwa ajili ya wengine katika dunia hii, pia Mandela ametufundisha kuwa na matumaini ya kile tunachokipigania badala ya kuwa waoga.

 Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Shabnam Mallick amesema Mandela hakuwa kiongozi wa Afrika pekee bali ni dunia nzima.

“Mandela kiongozi wa aina yake na mfano wa kuigwa katika wakati wetu, alipigania utu na usawa na pia kuchagiza ujasiri, wema na alikuwa tayari kujitolea uhuru wake na hata maisha yake kwa ajili ya wengine,” amesema.

Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Noluthando Mayende-Malepe amesema maadhimisho hayo ni muhimu kwa ajili ya kutambua jitihada zake katika kutatua migogoro, kukuza na kulinda haki za binadamu, usawa wa jinsia na haki za watoto na makundi mengine yaliyo hatarini; mapambano dhidi ya umaskini.

Pia amesema katika kumuenzi Mandela jamii inapaswa kuhakikisha inamlinda na kumsaidia mtoto kufikia ndoto zake kwani pamoja na mambo mengine Mandela alikuwa anapenda sana watoto na alifanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha ustawi wa mtoto kwenye upande wa elimu, afya na nyinginezo.

Amesema watoto wanakumbana na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuhatarisha ustawi wao ikiwemo kushindwa kwenda shule kutokana na kushindwa kupata vifaa vya kujihifadhia wakati wa hedhi kwa mabinti, umaskini, ukatili wa aina mbalimbali.

“Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela ni fursa kwa raia ulimwenguni kote kutambua uwezo wao binafsi na kuwa sehemu ya kuifanya dunia kuwa bora zaidi,” amesema.

Maadhimisho hayo pia yalisindikizwa na shughuli za kijamii, ikiwemo upakaji wa rangi, uandaaji wa chakula, upandaji wa miti pamoja na uchangaji wa fedha kwa ajili ya watoto wenye changamoto ya usonji katika kituo cha Victorious Center for Excellence kinachotoa tiba na elimu maalum kusaidia watoto wenye Usonji.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Sarah Laizer ametoa wito kwa jamii kutowafungia watoto hao ndani ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana katika jamii.

Amesema watoto hao wana haki sawa kama ilivyo kwa watoto wengine hivyo wawezeshwe ili waweze kuzifikia ndoto zao.

Vilevile ametoa wito kwa serikali na wadau wengine wa masuala ya watoto katika kuhakilisha elimu inatolewa zaidi ili kuondoa unyanyapaa kwa watoto hao.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts