Hatima kesi ya mauaji ya Milembe wa GGM kujulikana leo

Geita. Hatma ya washtakiwa wanne wanaodaiwa kumuua aliyekuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Milembe Suleman (43) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali itajulikana leo Julai 19, 2024.

Jaji Mfawidhi Kelvin Mhina anatarajia kutoa hukumu ya kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni, Dayfath Maunga (30), Safari Labingo (54), Genja Deus Pastory na Musa Pastory (33) ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka moja la kumuua Milembe kwa kukusudia.

Awali, washtakiwa hao waliokuwa watano walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Mei 24, 2023 na kusikilizaji wa shauri hilo Mahakama Kuu Kanda ya Geita ulianza Aprili 8, 2024 hadi Juni 28, 2024, pande zote mbili zilipomaliza kutoa ushahidi wake.

Upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 29 na vielelezo 19 na baada ya ushahidi wa Jamhuri Mahakama ilimwachia huru mshtakiwa wa tano, Cecilia Macheni baada ya kuona hana kesi ya kujibu.

Washtakiwa wanne waliobaki walijitetea wenyewe na wote kwa nyakati tofauti walikana kuhusika na mauaji hayo na kuiomba Mahakama iwaachie huru.

Shahidi wa pili na wa tatu katika kesi hiyo, waliieleza Mahakama namna simu za marehemu Milembe zilivyopatikana chooni baada ya mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory kuwapeleka mahali alikozitumbukiza.

Shahidi wa tano ambaye ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi PF 25416, Peter Joseph aliieleza Mahakama kuwa sampuli za alama za vidole alizopewa kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi zikiwa na alama A-A1na X-X1 zikiwa na jina la Genja Deus Pastory, zililingana kitabia na uhalisia wake na kidole cha kati cha mkono wa kushoto wa mshtakiwa wa tatu.

Shahidi wa sita katika kesi hiyo ambaye ni Ofisa Tabibu wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Christopher Matola aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Milembe, aliieleza Mahakama kuwa chanzo cha kifo cha Milembe kilitokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na majeraha makubwa ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri alieleza namna mshtakiwa wa kwanza, Dayfath Maunga (30) alivyowatafuta wauaji wa kumuua Milembe na kuwalipa Sh2.6 milioni kwa kazi hiyo.

Shahidi wa 13 aliieleza Mahakama namna mshtakiwa wa tatu, Genja Pastory alivyokiri kuumua Milembe na namna walivyofanikisha kufanya hivyo kwa kujifanya ni waganga wa kienyeji.

Kupitia maelezo yake onyo, mashtakiwa huyo alieleza kuwa Aprili 25, 2023 saa tatu asiku wakiendelea kuweka dawa kwenye nyumba alizokuwa akijenga Milembe eneo la Mwatulole, mshtakiwa wa tatu (Genja) alimtaka Milembe aliyekuwa na tochi achuchumae naye alitii, kisha akaanza kumkatakata na jambia sehemu mbalimbali za mwili na alizidiwa akaanguka, ndipo alikata tena sehemu za kichwani.

Shahidi wa 24, Koplo Hashimu aliieleza Mahakama namna walivyowakamata washtakiwa ambapo Mei mosi, 2023 walimkamata mshtakiwa wa kwanza Dayfath Maunga akiwa nyumbani kwa Milembe Usagara, Mwanza na baada ya mahojiano aliwaambia ili kuwapata wauaji wamtafute mtu aitwaye Safari Lubingo ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo.

Kukamatwa kwa Safari kuliwezesha kukamatwa pia kwa Musa Pastory ambaye ni mshtakiwa wanne aliyewasaidia kumpata Genja Pastory ambaye ilidaiwa baada ya kuua alikwenda kwa mganga wa kienyeji, Cecilia Macheni kuondoa mkosi.

 Shahidi wa 26 ambaye ni Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ally Kanenda aliieleza Mahakama namna vipimo vya vinasaba vilivyofanywa na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali vilivyobaini kuwa mpanguso wa damu kutoka kwenye mpini au mshikio wa jambia lililotumika kumuua Milembe ina uhusiano na mpanguso wa vinasaba vya mate vya mshtakiwa wa tatu Genja Pastory.

Wakitoa ushahidi wao kwa kuongozwa na mawikili wao, walidai kabla ya kukamatwa hawakuwahi kuonana na wala hawajawahi kuwasiliana kwa njia zozote za mawasiliano.

Dayfath Maunga, mshtakiwa wa kwanza alikiri kuishi nyumbani kwa Milembe lakini akadai alikuwa akifanya kazi ya kuuza duka la vipodozi la Milembe na kumsaidia kwenye biashara zake za kukopesha fedha kwa riba.

Mshtakiwa huyo alidai hahusiki na kifo hicho na hakuwa na sababu ya kufanya hivyo.

Mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo alidai hafahamiani na mshtakiwa wa kwanza na hakuwahi kuwasiliana naye na kuhusu kuwatafuta Musa na Genja  na kupanga njama za kumuua Milembe, alidai hawafahamu na hajawahi kuwasilina nao.

Mshtakiwa wa tatu, Genja Pastor alidai hakuwaonyesha polisi liliko jambia bali baada ya kumtoa kituoni walimchukua na gari na kumpeleka sehemu yenye nyasi nyingi na kumtaka atafute jambia na alipolipata aliulizwa kama analifahamu akadai halifahamu na kudai ushahidi uliotolewa mahakamani kuwa alichukuliwa alama za vidole si za kweli.

Kwa upande wa mshtakiwa wanne Musa Pastory alidai hakuwahi kutoa maelezo polisi na wala hakuwahi kuwataja washtakiwa wengine popote, kwa kuwa hakuwa anawafahamu.

Alidai hajawahi kuhusika na mauji ya Milembe na kuiomba Mahakama imuachie huru.

Endelea kufuatia mitandao ya Mwananchi kupata kitakachojiri mahakamani leo.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts