Sungusia aeleza Kamati ya Maadili TLS inavyoingilia masilahi ya mawakili

Dar es Salaam. Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Harold Sungusia amesema miongoni mwa mambo yaliyomsumbua katika uongozi wake wa mwaka mmoja ni Kamati ya Maadili ya Mawakili, akisema inaingilia masilahi ya wanataaluma hiyo.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi amesema kamati hiyo imeundwa kisheria, hivyo kama ni ubovu wa sheria ndio ufanyiwe kazi.

Miongoni mwa mawakili waliokumbana na mkono wa kamati hiyo ni pamoja na aliyekuwa Rais wa TLS, Fatma Karume (2018-2019), aliyevuliwa uwakili Septemba 23, 2020 kutokana na malalamiko ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Adelardius Kilangi kuwa alitumia lugha ya kumdhalilisha alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu katika kesi ya kumshtaki Rais na AG

Hata hivyo, Juni 21, 2020 Mahakama Kuu ilitengua uamuzi huo wa Kamati ya Maadili.

Mwingine aliyefikishwa katika kamati hiyo ni Boniface Mwabukusi ambaye Mei mwaka huu alikutwa na hatia na kupewa onyo.

Naye wakili Peter Madeleka, alifikishwa lakini amefungua kesi Mahakama Kuu kuipinga kamati hiyo.

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya TLS kufanya mkutano mkuu ambao pamoja na mambo mengine utafanya uchaguzi wa kupata viongozi wapya akiwamo rais, Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Sungusia Julai 17, 2024.

Sungusia aliyeingia madarakani Mei 2023, anatarajiwa kukabidhi kijiti kwa miongoni mwa wagombea watano ambao ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda na Sweetbert Nkuba atakayeibuka mshindi.

Wagombea hao watachuana katika uchaguzi utakaofanyika Agosti 2, 2024 jijini Dodoma.

Sungusia akigusia kamati ya maadili ya mawakili, amesema, “Miongoni mwa mambo tuliyozungumzia Siku ya Sheria Februari mwaka huu na Jaji Kiongozi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni suala la Kamati ya Maadili.

“Katika mambo tuliyosema hadharani ni kwamba, mpaka sasa huwezi kujua ofisi ya kamati hii iko wapi, hata ukitaka kupeleka nyaraka kwenye hiyo kamati, utapeleka kwa Msajili, lakini ukitaka kukutana na kamati huwezi kujua ofisi yao iko wapi,” amesema huku akieleza suala hilo lilikuwa miongoni mwa ajenda zake alipoingia madarakani.

Ametoa mfano wa kesi ya wakili Mpale Mpoki aliyefungiwa uwakili kwa miezi sita alipokuwa akimtetea wakili Boniface Mwabukusi kwenye kamati hiyo mwaka huu, akisema walipotaka kukutana na kamati hiyo, ili wapate mwenendo wa shauri pamoja hukumu yake, ilishindikana.

“Utakuta mheshimiwa jaji labda yuko Mwanza, katibu mwenyewe labda yuko Dar es Salaam, yaani hakuna ofisi rasmi ya hii kamati,” amesema.

Kuhusu sheria, Sungusia amesema idadi kubwa ya wajumbe wa kamati hiyo ni watumishi wa umma na Mahakama, huku mawakili wakipewa nafasi moja.

“Kwa mfano, Kenya idadi kubwa inakuwa ni mawakili wenyewe, kwa nini huku kwetu idadi kubwa inatoka kwenye sekta ya umma na sio mawakili wenyewe? Kwa hiyo ndio changamoto tulizonazo,” amesema.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, walidhamiria kufanya mkutano wa kuijadili na kuichukulia hatua.

“Tukaandaa mkutano wa dharura Desemba 15, 2023, tukaletewa order (amri) usiku kwamba hakuna kufanya huo mkutano.

“Kuna mwanachama mwenzetu alikimbilia mahakamani akaenda akafungua kesi kuzuia mkutano usifanyike. Sijui alikuwa na masilahi gani, lakini kufungua kesi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.”

Amesema suala hilo litajadiliwa kwenye mkutano mkuu wa mwaka huu.

Alipoulizwa kuhusu malalamiko ya TLS, AG Feleshi amesema kamati hiyo imeanzishwa kisheria.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mawakili Sura ya 341, kifungu cha 4(1) inataja kuanzishwa kwa Kamati ya Mawakili, ikijumuisha Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano aliyechaguliwa na Jaji Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Naibu Mwanasheria Mkuu au Mkurugenzi wa Mashtaka, Wakili anayeendelea na kazi aliyetajwa na Baraza la Chama cha Wanasheria.

Kifungu cha 4(4) kinasema Jaji wa Mahakama Kuu atakuwa mwenyekiti wa Kamati na ataongoza mikutano yote ya Kamati na wakati wa kutokuwepo kwa Jaji wa Mahakama Kuu aliyechaguliwa na Jaji Mkuu ama chini ya kifungu cha (1) au kifungu cha (3), Mwanasheria Mkuu, Naibu Mwanasheria Mkuu au Mkurugenzi wa Mashtaka, atakuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Kifungu kidogo cha (5) kinasema, wajumbe wawili wa Kamati, mmoja wao akiwa Mwanasheria Mkuu au Naibu Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka wataunda kolamu.

“(6) Swali lolote mbele ya kamati litakaloamuliwa kwa kura nyingi za wajumbe waliopo.”

Kuhusu mikutano na mahali pa kukutaniani Kifungu cha 5 kinasema: “Mikutano ya kamati itafanyika katika nyakati na maeneo yatakayowekwa na Mwanasheria Mkuu.”

Dk Feleshi aliyewahi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu amesema pamoja na sheria hiyo kuunda kamati, bado sheria inaweza kubadilishwa.

“Kwenye sheria hakuna siasa, kama sheria haifai, inarekebishwa,” amesema.

Mbali na Sheria ya TLS, amesema kanuni za maadili za mawakili zinaunda kamati ya maadili ndani ya chama hicho.

 “Unavyoona muundo ulivyo leo, yawezekana kweli inahitaji uboreshwaji, lakini unapoona mwenyekiti wa kamati ni Jaji ujue kwamba Jaji Mkuu ndiye anayewasajili mawakili. Ujue pia Jaji Mkuu kupitia Mahakama mawakili wanapata leseni,” amesema.

Amesema kamati kama hiyo haipo kwa mawakili pekee:“Sheria ya Utawala wa Mahakama kifungu cha 37 na uendelea kuna Kamati ya Majaji, kifungu cha 41 Kamati ya Maadili ya maofisa wa Mahakama, Kifungu cha 50 na 51 Kamati ya Maadili za Mahakama na wenyeviti wake ni wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Kwa hiyo suala la maadili sio kitu kidogo.”

Katika muundo wa kamati hiyo, amesema mjumbe wa TLS anaingia, ili kulinda masilahi ya mawakili.

Wakati akiingia madarakani, miongoni mwa mambo aliyoahidi kuyafanya ni kupigania mchakato wa Katiba, kuongeza mapato ya chama na kukabiliana na changamoto za kimaadili kwa mawakili kwa kuwabana zaidi mawakili vishoka.

Sungusia ameeleza jinsi alivyotekeleza ahadi zake akisema ameacha mkakati wa kufikia kwenye mabadiliko ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Falsafa yangu ni kwamba, hatuhitaji kuandaa Katiba kama chombo cha kusuluhisha migogoro, bali Katiba inayopatikana katika mazingira ya amani kwa ajili ya kuleta maendeleo,” amesema.

Ametaja nchi za Ethiopia, Uganda, Kenya na Afrika Kusini, akisema Katiba zao zilitokana na machafuko au kupambana na ukoloni.

Kuhusu kuukwamua mchakato wa Katiba, amesema TLS wamejiuliza jinsi ya kuanza mchakato huo.

“Nakumbuka aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro (sasa Waziri Utamaduni, Sanaa na Michezo), alisema tunahitaji miaka mitatu ya kutoa elimu ya Katiba. Waziri anazungumza vile, lakini hajawauliza wananchi.

“Sisi tunawauliza wananchi mnataka tuanzie wapi? Kwa sababu mwaka 2014 tulikwama ule mchakato wa Katiba,” amesema na kuongeza ndani ya kipindi chake amefanya makongamano matano ya Katiba katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha na Dodoma.

“Majibu tuliyopata ni kwamba tulikwama kwa sababu kuna ajenda tulikuwa hatujazifanyia kazi vizuri, mfano kulikuwa na ajenda ya Muungano, wengine walikuwa wanasema Serikali mbili, tatu, nne au mkataba,” amesema. 

Baada ya midahalo hiyo, amesema wameunda kamati ya wataalamu itakayoendeleza mawazo hayo ya wananchi, ili twende mbele.

“Shida tuliyokumbana nayo ni muda mfupi wa uongozi wetu, tumekuwa na muda wa miezi minane tu ya kufanya kazi kwa sababu ile miezi miwili ya kwanza ilikuwa ni ya kujiandaa kukaa ofisini na hii mwili ya mwisho ni kujiandaa na uchaguzi,” amesema.

Hata hivyo, amesema suala hilo limewekwa kwenye mpango mkakati wa TLS, hivyo hata uongozi unaokuja utalazimika kuutekeleza.

Amesema katika mambo waliyosisitiza katika kamati hiyo ni mgongano wa masilahi.

“Wanaotunga Katiba wasitumie huo mchakato kujitengenezea ulaji mbele, kwa hiyo lazima tuweke vigezo vya mtu atakayeshiriki kwenye mchakato wa Katiba asije akagombea nafasi za uongozi, ili asije akawa na mgongano wa masilahi,” amesema.

Mabadiliko ya sheria ya TLS, kwa sasa viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 2, 2024, watakaa madarakani kwa miaka mitatu.

Akieleza mambo anayojivunia katika uongozi wake, Sungusia amesema ni kutatua changamoto ya watumishi wa TLS kutolipwa mishahara kwa wakati. 

“Tangu tulipochaguliwa Mei 2023 tumeingia ofisini, kitu cha kwanza kilichokuwa kinakera sana hapa TLS ni wafanyakazi kupitisha miezi miwili mitatu mpaka mitano bila kulipwa mshahara.

“Katika uongozi wangu, hakuna hata mwezi mmoja ambao wafanyakazi hawakulipwa mshahara. Kwa hiyo jambo la kwanza kabisa ni haki za wafanyakazi,” amesema. 

Jambo la pili, amesema ni kufanikisha marekebisho ya Sheria ya TLS baada ya kuwatembelea viongozi wa Serikali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria na Spika wa Bunge.

“Kwa hiyo sheria ilibadilishwa, japo ilikuwa na ukakasi kwa sababu kuna vitu viliingizwa ambavyo hatukuviomba.

“Tulipendekeza muda wa mtu kukaa madarakani iwe miaka mitatu au miwili, Serikali ikakubali, Bunge likapitisha miaka mitatu,” amesema Sungusia.

Kuhusu vishoka, amesema walipendekeza faini iongezwe kutoka Sh2,000 na sasa imekuwa Sh20 milioni na badala ya kifungo cha miezi 12 sasa itakuwa miezi mitatu au vyote viwili.

Related Posts