Kwimba. Mahakama ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza imemuhukumu mkazi wa Mtaa wa Majengo mjini hapa, Michael John (45), kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kambo.
Binti huyo mwenye umri wa miaka 14, ni mwanafunzi wa kidato cha pili.
Akitoa ushahidi Julai 17, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, John Jagadi, mtoto huyo alisema baada ya mama yake kufariki dunia mwaka 2020, aliendelea kuishi na baba huyo na ilipofika mwaka 2022 alianza kumwingilia kimwili.
“Baada ya kufariki mama yangu mzazi mwaka 2020, niliendelea kuishi na baba yangu ambaye hakunizaa, alianza kunibaka mwaka 2022 tukiwa Rorya, Mara na alikuwa akinitishia kunipiga na kunifukuza kama nitasema,” alieleza mtoto huyo mbele ya mahakama.
Akijitetea mahakamani hapo, Michael amesema baada ya mke wake kufariki dunia wakiwa Rorya, Mara, walihamia Mtaa wa Majengo, Ngudu wilayani Kwimba walikopanga vyumba viwili.
Baadaye, amesema alirudisha chumba kimoja kwa kuwa hakuwa na fedha za kulipia vyumba viwili, ndipo akaanza kulala chumba kimoja na mtoto huyo.
Pamoja na kulala chumba kimoja, amesema hakuwahi kumwingilia kimwili binti huyo.
Hata hivyo, mahakama ilikubaliana na upande wa mashtaka uliothibitisha kosa bila kuacha shaka na kumtia hatiani.
Alipotakiwa aeleze kwa nini isimpatie adhabu kali kutokana na kosa hilo, mshtakiwa alisema:
“Mheshimiwa hakimu, naiomba Mahakama inipunguzie adhabu, ninategemewa na huyu binti ambaye anasoma sekondari kidato cha pili,” aliiambia Mahakama.
Baada ya maombi hayo, mahakama iliyatupilia mbali na kumuhukumu kwenda jela miaka 30 ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Awali, Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Juma Kiparo akimsomea mshtakiwa mashtaka ya kubaka mtoto huyo akiwa na miaka 12 kinyume cha sheria.
Kiparo alidai Michael alipohamia Ngudu Mtaa wa Majengo Barabara ya Nyambiti Machi 2023, aliendelea kufanya mapenzi na mtoto huyo.
“Lakini mama yake mkubwa na mtoto huyo alipopata taarifa, alimfuata na kumkanya baba huyo na alimwambia mtoto huyo kama baba yake atamtaka tena amkatalie, lakini mtuhumiwa aliendelea,” alisema Kiparo
Alidai siku mtoto huyo alipomkatalia baba huyo alimpiga, ndipo akaenda kumweleza mama yake mkubwa kuwa kapigwa kwa sababu alikataa kufanya naye mapenzi.
Mwendesha mashtaka huyo alidai baada ya hatua hiyo, mama yake huyo mkubwa alitoa taarifa polisi na mshtakiwa akakamatwa.