Shambulio la droni laua mmoja Tel Aviv – DW – 19.07.2024

Mamlaka za Israel zimesema kuwa shambulio hilo lilitokea mjini Tel Aviv saa tisa alfajiri. Afisa wa jeshi hilo ambaye hakutaka kutajwa jina amesema droni iliyoshambulia ilitambuliwa na mfumo wa ulinzi lakini king’ora cha tahadhari hakikulia kutokana na makosa ya kibinadamu.

Idara ya huduma za dharura nchini humo imesema, watu karibu kumi walipata usaidizi kutoka kitengo hicho na wengine walipelekwa hospitali kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha madogo yaliyosababishwa na shambulio hilo.

Soma zaidi: Israel: Watu wanane wajeruhiwa katika shambulio la gari katika mji wa Tel Aviv

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagar, amesema  wanaamini kuwa droni iliyotumika katika tukio hilo imetengenezwa Iran na ilirushwa kutokea Yemen. Kundi la waasi wa Kihuthi la nchini Yemen, limetangaza kufanya shambulio hilo.

Bunge la Israel lapinga kuundwa kwa dola la Palestina

Katika hatua nyingine, bunge la Israeli limepinga kwa sauti moja wazo la kuundwa kwa dola la Kipalestina, katika kura iliyopigwa Alhamisi. Azimio lililotolewa na bunge hilo limesema kuwa kuundwa kwa taifa la Palestina katikati ya ardhi ya Israel kutasababisha uwepo wa hatari kwa taifa la Israel na raia wake. Limeongeza kuwa hatua hiyo itachochea mzozo na kuudhoofisha ukanda huo.

Shambulio la droni mjini Tel Aviv
Wakaazi wa Tel Aviv wakishuhudia gari lililoharibiwa kwa shambulio la droniPicha: Ricardo Moraes/REUTERS

Soma zaidi: Baraza la Usalama lapitisha azimio la kulaani mashambulizi ya Wahouthi

Hayo yanajiri wakati mahakama ya juu zaidi katika Umoja wa Mataifa ikjipanga hii leo kutoa maoni yake juu ya uhalali wa Israel kuyakalia kuyakalia kwa mabavu maeneo ya Palestina. Maoni hayo hata hivyo hayana nguvu kisheria. Lakini kama majaji wa mahakama ya The Hague wataamua kuwa Israel imevunja sheria ya kimataifa, hatua hiyo itaongeza shinikizo la kisiasa kwa Israel.

Katika hatua nyingine, kiongozi wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas anatarajiwa kuelekea Urusi  Agosti 13. Kulingana na shirika la habari la serikali la Urusi, RIA, Abbas anatarajiwa kukutana na Rais Vladimir Putin

 

Related Posts