Serikali yakubali yaishe baada ya mgomo wa wafanyabiashara Holili

Rombo. Wiki moja baada ya wafanyabiashara wa nafaka katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kugoma kwa sababu ya ongezeko la ushuru katika mpaka wa Holili na Tarakea kutoka Sh50,000 hadi Sh300,000, Serikali imekubali yaishe na biashara zimerejea kama kawaida kwa kutoza viwango vya awali.

Julai 12, 2024 baada ya wafanyabiashara hao kutangaziwa ushuru huo mpya, waligoma na kufunga barabara ya Holili – Moshi kwa zaidi ya saa mbili wakishinikiza halmashauri ya wilaya hiyo kufuta ushuru wa Sh300, 000 kwa kila gari lenye mzigo wa mahindi, linaloingia katika soko la Holili na Tarakea.

Hali hiyo ilimlazimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala kufika katika maeneo hayo na kuzungumza na wafanyabiashara hao na kuzuia ushuru huo kwa muda hadi mwafaka wa jambo hilo utakapofikiwa.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake, Mwangwala amesema wamekaa meza moja ya mazungumzo na wafanyabiashara hao na wamekubaliana ushuru utakaotolewa ni ule wa awali na biashara zitafanyika kama kawaida.

Amesema maelekezo aliyotoa kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhusu tatizo lililojitokeza, ni kwamba wafanyabiashara hao hawakupata taarifa kwa usahihi kuhusu bei hiyo mpya ya ushuru.

 “Nashukuru vikao vilifanyika Jumatatu na Jumanne na wamekubaliana vizuri tu, kimsingi ule ushuru ambao ulikuwa unatozwa awali wa Sh50, 000 ndio utakuwa unaendelea kulingana na mazingira yalivyo,” amesema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wilayani ya Rombo, Godfrey Mwaiyo amesema hali hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara na imekuwa ikiwakera wafanyabiashara na hivyo akaiomba Serikali kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano na wafanyabiashara ili kuondoa changamoto hizo.

“Tunaishukuru serikali ya wilaya kwa kuwa sikivu, kwa kushughulikia changamoto hii mara moja, tumekubaliana sasa turudi kwenye hali ile ya kawaida ya kufanya biashara kama ilivyokuwa hapo awali,” amesema Mwaiyo. 

Kwa upande wake, Sesilia Peter, mmoja wa wafanyabiashara wa Tarakea, ameishukuru Serikali kwa kuwaondolea vikwazo vilivyowekwa na kuwawezesha kuendelea na biashara zao kama kawaida.

“”Leo biashara zimeanza upya vizuri na changamoto zote na vikwazo vyote barabarani vimeondolewa, kwa hiyo wafanyabaishara kwa sasa tuko vizuri tunashukuru sana,” amesema mfanyabiashara huyo.

Mfanyabiashara mwingine, Richard Charles amesema changamoto ilijitokeza iliwagharimu kutokana na biashara zao kusimama kwa muda.

“Tunamshukuru mwenyekiti wetu wa Jukwaa la Wafanyabiashara kwa kutuweka pamoja na kuzungumza na mamlaka na mwisho wa siku wakatuondolea vikwazo,” amesema mfanyabiashara huyo wa mahindi.

Related Posts