Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema demokrasia ya Afrika bado ina changamoto kwenye eneo la uchaguzi na hivyo ametoa wito kwa vyama vya upinzani kuona haja ya kudumisha uhusiano baina ya nchini na nchi ili kuondosha udhalimu huo.
Amesema chaguzi nyingi barani hapa hutawaliwa na mizengwe inayochezwa na vyama tawala, hali inayoondoa dhana ya demokrasia inayoheshimu maamuzi ya wananchi kupata viongozi.
Kiongozi huyo ameyazungumza hayo leo wakati akipokea ugeni wa Chama kikuu cha upinzani Malawi, Democratic Progressive Party (DPP) kwenye ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaama.
Ugeni wa DPP, umeongozwa na Makamu wa Rais wa chama hicho, Dk George Chaponda aliyeambatana na Mkuu wa Operesheni na Mbunge wa Bunge la Malawi, Charles Mchacha.
“Demokrasia ya Afrika bado ina changamoto kubwa kwenye chaguzi zetu, ni muhimu kudumisha mahusiano ili tuweze kuungana na kuendelea kuona namna bora ya kuondosha udhalimu kwenye uchaguzi na kufikia umajumui wa Afrika tuutakao,” amesema Semu aliyekuwa na wake (Bara), Isihaka Mchinjita
Semu amegusia pia namna ACT Wazalendo inavyoendelea kuwa mstari wa mbele kuendeleza utawala bora wenye kuheshimu misingi ya demokrasia na kutekeleza kwa vitendo madai ya mabadiliko kwa kushiriki michakato na wakati mwingine kwenda mahakamani.
Katika mazungumzo hayo, Dk Chaponda amesema wanajua changamoto iliyopo na kikubwa wamejifunza ni kuepuka migogoro ya ndani ya chama kwani ni jambo ambalo haliwezi kuwapa ushindi bali kupoteza.
“Lengo ni kuona nani mnapaswa kushughulika naye kwa masilahi mapana ya wananchi na chama. Migogoro ya ndani haina afya na itawasambaratisha,” amezungumza alipokuwa akitoa uzoefu na wenzake walipoondolewa serikalini na kujikuta wamekuwa chama cha upinzani.
Katika hatua nyingine, Dk Chaponda amegusia siri ya mafanikio ya kushinda uchaguzi ni kubeba agenda za umma na kuzishikilia bila kuchoka na kuachana na mlolongo wa agenda zinazoweza kuwapoteza wananchi na kushindwa kuwaelewa.
Akizungumzia namna ACT Wazalendo ilivyojipanga, Semu amesema wameanzisha mfumo mpya wa kusajili wanachama kidijitali.
“Julai 22, 2024 chama kinazindua programu maalumu ya kusajili wanachama milioni 10 kwa miezi 10 hii ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mtandao wa chama na kujiandaa vyema kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2025,” amewaambia wageni hao.