Milan. Mwandishi wa habari kutoka Milan nchini Italia, Giulia Cortese amehukumiwa kulipa faini ya Euro 5,000 sawa na Sh14.6 milioni kwa kosa la kumdhihaki Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Giorgia Meloni.
Mahakama imeeleza kuwa Cortese alitenda kosa hilo mtandaoni kwa kuchapisha ujumbe kwenye mtandao wa X, akisema Waziri huyo ni mdogo na hawezi hata kumuona, jambo ambalo lilitafsiriwa kama kitendo cha dharau na kufedhehesha maumbile kutokana na chapisho hilo.
Tovuti ya The Guardian imesema Cortese mwenye umri wa miaka 36, alichapisha picha ya Waziri Mkuu Meloni akiwa na Benito Mussolini kwa nyuma katika mtandao ambao zamani uliitwa Twitter.
Akijibu kitendo cha Cortese, Waziri Mkuu Meloni kupitia mtandao wa Facebook alisema picha iliyochapishwa na mwandishi huyo ni potofu kisha akamuagiza mwanasheria wake kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwandishi huyo.
Akijibu mapigo, Cortese ameandika: “Njia ya vyombo vya habari uliyounda kwenye ukurasa wako wa Facebook inakufaa kwa jinsi ulivyo: mwanamke mdogo, hunitishi Meloni. Baada ya yote, una urefu wa mita 1.2 tu (futi 4). hata siwezi kukuona”
Hata hivyo, Cortese hajakutwa na hatia kwa ujumbe wake wa kumlinganisha Meloni na Mussolini, lakini alipatikana na hatia ya kashfa, jambo ambalo hakimu wa Milan amesema ni sawa na kuaibisha mwili.
Kufuatia hukumu hiyo, Cortese amesema maneno ya utani imekuwa kashfa. Hivyo hana uhuru tena wa kuandika kuhusu Serikali, kwa sababu amekwishatambuliwa kama mwandishi wa habari usiyefaa kwa Serikali na yenyewe hairuhusu chochote.
Hata hivyo, kulingana na vyombo mbalimbali vya habari vya Italia, Waziri Mkuu Meloni ana urefu wa mita 1.63 na si mara ya kwanza kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwandishi wa habari au mtu ambaye anayemkosoa hadharani.