KWA miongo mingi sasa umekuwa utamaduni wa klabu kufanya kambi za kujiandaa na msimu mpya maarufu kama pre season.
Kwa miaka ya karibuni, kalenda za ligi ya soka duniani hazitofautiani sana, yaani ligi zinaanza na kutamatika katikati ya kalenda ya mwaka.
Ligi za mataifa mengi zinaanza Agosti au Septemba na kutamatika Mei au Juni. Baada ya ligi kufikia mwisho, wachezaji uchukua likizo ya mwaka kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine.
Likizo inapokwisha, wachezaji hawaanzi kucheza moja kwa moja bali huandaliwa kimwili, kiakili na kiufundi tayari kuukabili msimu mpya.
Maandalizi ya msimu au pre-season ni kipindi cha wachezaji kurudi katika utimamu baada ya likizo na mambo yatokanayo na likizo kama kuongezeka uzito. Ni kipindi cha wachezaji kuonyesha kiwango chao kwa makocha na kipindi cha makocha kueleza falsafa zao kwa wachezaji wageni au kocha mgeni kujitambulisha kwa timu mpya.
Hiki ndiyo kipindi cha walimu kuwajua wachezaji uwezo na tabia na kufanya maamuzi nani atatumika namna gani. Msimu unapoanza walimu wanakuwa na mambo mengi na hawana muda wa kuangalia vitu vidogo vidogo.
Kipindi hiki cha kujiandaa na msimu ni kipindi mwafaka kucheza michezo ya kirafiki. Mara nyingi timu hutafuta michezo laini kwanza, kisha michezo yenye ushindani wa kiwango kilekile cha mashindano yanayowakabili.
Matokeo katika kipindi hiki huwa si jambo la muhimu kwa walimu lakini kwa mashabiki bado hufuatilia timu inavyofanya ili kujipima nafasi yao katika msimu mpya unaosubiriwa.
Katika miaka ya karibuni na kadri mpira unavyovutia uwekezaji, klabu zimekuwa vikiweka kambi za pre-season mbali kabisa na nyumbani labda kwenye mataifa ya kigeni ambako kuna miundombinu mizuri ya kambi, utulivu na uwezekano wa kupata michezo ya kujipima nguvu. Pre-season pia imekuwa sehemu ya biashara hasa katika kutangaza wadhamini na hata klabu kujitangaza zenyewe. Mathalani, msimu huu ukiangalia ratiba ya timu ya Arsenal ya Uingereza imeenda marekani ambako itaweka kambi nakucheza michezo ya kirafiki iliyodhaminiwa na kampuni kubwa za huko. Mataifa ya Asia kama China, Korea na Japan pia yamekuwa na utamaduni wa kuunganisha nguvu za kampuni na kuzialika klabu kubwa kama Manchester United, Arsenal, Manchester City, Real Madrid, PSG, Barcelona na nyinginezo kuweka kambi huko, hivyo klabu zinapata pre-season na fedha za kutosha. Michezo mingine ya Pre-season huwa ni sehemu ya mkataba wa udhamini, mfano ni mashindano ya Emirates yanayohusisha timu zinazodhaminiwa na shirika la ndege la Emirates.
Hapa nyumbani, utaratibu wa kwenda pre-season nje ya nchi haujaanza leo. Miaka ya 1970 na 1980 timu za Yanga na Simba zilifanya ziara za nje kama Ulaya na Brazil na kuweka kambi huko. Hata hivyo, kwa miaka ya karibuni, ni Yanga iliyoanza utamaduni wa kwenda pre-season nje ya nchi.
Yanga chini ya marehemu Yusuf Manji iliweka kambi kule Antaliya Uturuki ambako pia ilipata michezo kadhaa ya kirafiki. Baada ya hapo imekuwa ni kama kawaida kwa timu za hapa nchini zikiongozwa na Simba kuweka kambi katika mataifa ya kigeni hasa ukanda wa mashariki ya kati kama Misri na Uturuki. Azam msimu uliopita iliweka kambi Tunisia.
Mwaka huu tayari Simba iko Misri ikiwa na kocha mpya na baadhi ya wachezaji wapya. Yanga imeweka kambi Avic Town, Kigamboni ikiwa ni kwa miaka miwili mfululizo bila kutoka nje ya nchi na ikanyakua ubingwa mbele ya Azam na simba waliokuwa wameweka kambi ugenini.
Hata hivyo, Yanga imesafiri kwenda Afrika ya Kusini na itaweka kambi na kucheza michezo kadhaa ya kujiandaa na msimu.
Maandalizi ya msimu kwa hapa nyumbani yanaweza kuwa kielelezo cha uchumi wa klabu. Sio kila klabu ya Ligi Kuu ina uwezo wa kuweka kambi ya muda mrefu au ya nje ya nchi. Azam, Simba na Yanga zinaonekana kuwa na ligi ya kwao.
Gharama za kambi ya timu kwa kiasi fulani zinaweza kutafsirika katika matokeo na msimamo wa Ligi Kuu. Klabu hizi tatu zinaonekana kuwa na ligi yao kifedha na ligi yao kimpira. Nafasi tatu za juu zimekuwa chini ya umiliki wa klabu hizo, huku nafasi ya nne ikibadilishana mikono miongoni mwa kiabu 12 zilizobaki.
Pre-season ni muhimu kwa kila timu na kwa kila mwanamichezo, lakini ni aina gani ya pre-season na gharama yake inategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa kifedha na hata mtandao ilio nao klabu husika.
Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kwenye simu yake hapo juu.