Wakulima waelezwa athari kununua karafuu kwa vishoka

Pemba. Wakulima wa karafuu Kisiwani Pemba, wametakiwa kutouza karafuu zao kwa watu wanaopita mitaani kwani jambo hilo licha linakwenda kinyume na sheria ya maendeleo ya karafuu Zanzibar linawafanya wadhulumiwe kwani vipimo hivyo ni vya wizi.

Akizungumza na waandishi wa habari huko katika ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi Chake Chake. 

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Sudi Said Ali amesema vipimo vinavyotumia na walanguzi hao vina ujazo mkubwa ukilinganisha na pishi ya kawaida.

Amelzimika kutoa kauli hiyo Julai 19, 2024 bada ya kubaini kuwapo vipimo hivyo wakiwa katika harakati zao za kukagua zao la karafuu katika msimu huu.

“Kuna watu wasiopendelea maendeleo ya mkulima wamekuwa wakipita mitaani na kununua karafuu zao kinyume na sheria na kwa kutumia vipimo visivyo sahihi,” amesema. 

Akitolea mfano pishi walizozikamata kwa walanguzi wanaopita kununua karafuu kwa wananchi Mkurugenzi huo amesema moja ni sawa na kilo mbili, na nyengine kilo mbili kasorobo huku kipimo cha pishi halali ya karafuu ni kilo moja na robo.

“Wakati tukiwa katika harakati zetu za kupitia maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Chake Chake na Mkoani kuangalia maendeleo ya zao hilo kwa wakulima tumebaini kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipita mitaani kununua karafuu kwa wananchi wakati shirika hadi sasa hadija fungua zozezi la ununuzi wa zao hilo,’’ amesema Sudi.

Sudi amesema Shirika hilo limekuwa likichukua juhudi za makusudi katika kuwapatia wakulima miche ya zao hilo kwa ajili ya kuimarisha zao hilo lakini juhudi hizo zinashindwa kufikiwa kutokana na baadhi ya wananchi kuhajumu zao hilo.

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wakulima hao kutouza karafuu zao kwa mtu yeyote kwani shirika halijamtuma mtu kwa ajili ya kuwanunulia karafuu na kueleza kuwa wakati huu wakisubiri kuzinduliwa kwa msimu mpya wa karafu.

Amesema shirika hilo kwa kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya wataendelea kuwafuatilia wale wanaopita kwa wananchi na kuwahadaa ili wawauzie karafuu na wale ambao watakamatwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Ofisa Mdhamini wa Shirika hilo Kisiwani Pemba, Abdalla Ali Ussi alisema limekuwa likiwapitia wakulima na kuwakumbusha kujiepusha kujihusisha na uhujumu wa zao hilo.

Baadhi ya wakulima akiwemo Soud Kombo amesema wakati mwingine wanauza kwa watu wa mitaani kwani wao hutoa fedha wakati huohuo tofaui na shirika fedha zao hupitia kwenye mifumo hivyo kuchukua muda mrefu kupata fedha hizo.

Related Posts