Unguja. Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman, amesema ili kuzitatua changamoto za wavuvi na uharibifu wa mazingira ya baharini, lazima kuwepo ushirikiano wa pamoja kati ya viongozi wa Mikoa, Wilaya na Masheha.
Kauli hiyo inakuja kutoana na ukweli kwamba kumekuwa na uharibifu mkubwa unaofanyika katika maeneo tengefu ya bahari sambamba na kukithiri kwa uvuvi haramu nchini.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja leo Ijumaa Julai 19, 2024 kujadili namna ya kutatua changamoto za wavuvi juu ya matumizi mabaya ya zana za uvuvi zisizokubalika kisheria.
Waziri Shaaban alisema Serikali ipo mbioni kutoa boti kubwa zenye vifaa kamili kwa wavuvi wa kijiji cha Chwaka ili waondokane na uvuvi waliouzoea na kuvua kisasa, lengo kuimarisha uhifadhi wa bahari na rasilimali zake.
“Ni vyema wavuvi muwe tayari kukubaliana na maamuzi ya Serikali kwa kuacha uchafuzi wa mazingira katika maeneo tengefu pamoja na uvuvi haramu unaorejesha nyuma juhudi zetu za kuimarisha ukuaji wa uchumi nchini,” alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema viongozi hao wanaunga mkono hatua ya Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kuwapatia boti wavuvi inayolenga kutatua changamoto zilizomo katika shehia hiyo.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wa sekta nyingine kutoa ushirikiano wa pamoja ili kujenga imani za wananchi na kukuza uchumi wao.
Mkuu wa Wilaya ya Kati, Sadifa Juma Khamis, aliwasisitiza wavuvi kufuata utaratibu uliowekwa ili kuondoa migogoro inayojitokeza mara kwa mara kati yao na Serikali.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Chwaka, Haji Makame Mlenge, aliiomba Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kufanya haraka kukamilisha taratibu za kuwapatia wananchi mikopo nafuu ya boti ili waondokane na uvuvi katika maeneo tengefu ya bahari pamoja na matumizi ya zana zisizokubalika kisheria.
Baadhi ya wavuvi wamesema elimu zaidi inahitajika kutolewa kwa watumiaji wa bahari ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa na kupata ufanisi unaotarajiwa.
“Bado elimu inahitajika ili kujua umuhimu wa kutunza mazingira na athari za uvuvi haramu, pia kuwapo na ushirikishwaji,” alisema mvuvi Amour Suleiman.