Mwanga. Wazazi katika Kata ya Kigonigoni iliyopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia upungufu wa walimu ikielezwa baadhi ya shule za shule za msingi zenye watoto wengi zina walimu wawili hadi wanne.
Wilaya hiyo yenye shule za msingi 110, ina jumla ya wanafunzi 24,476 wa darasa la awali hadi la saba na hivyo kuwa na uhitaji wa walimu 1,027.
Wakati mahitaji ya walimu yakiwa 1,027, waliopo ni 650 na hivyo kuacha upungufu wa walimu 377, na hivyo kusababisha wachache waliopo kubeba mzigo mkubwa wa masomo.
Wakizungumzia upungufu huo, baadhi ya wazazi wenye watoto katika shule hizo, wamesema changamoto hiyo pia umesababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kufanya vuzuri kwenye mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi.
Omary Idd, mkazi wa Kata ya Kigonigoni, amesema changamoto ya walimu, hususan kwa shule za pembezoni, wamekuwa wakiizungumza mara kwa mara wanapokuwa kwenye mikutano na viongozi lakini bado haijapatiwa ufumbuzi.
“Shule zetu za msingi hapa walimu ni wachache, mfano ukiangalia shule yetu ya msingi Kwakihindi walimu ni wawili na wanafunzi wanakaribia 200 darasa la awali hadi la saba, lakini shule ya Ruru nayo ina wanafunzi 200 lakini walimu watatu. Ukitafakari mzigo wanaoubeba walimu, kweli ni changamoto,” amesema Idd.
Ameongeza kuwa: “Pia, ipo shule ya Kigonigoni ina wanafunzi 417, lakini walimu wapo wanne akiwemo mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa la awali, hili pia linaathiri watoto wengi kitaaluma,” amesema Idd.
Abtway Kajiru amesema upungufu wa walimu ni kikwazo cha maendeleo ya kitaaluma kwa wanafunzi na ameomba Serikali iliangalie suala hilo kwa uzito kwa kuwa wanaoteseka ni wale wa maeneo ya vijijini.
“Unakuta walimu ni wachache halafu watoto ni wengi, hii inaathiri sana wanafunzi na kuwafanya wasifanye vizuri kitaaluma na wengine wanafaulu kwenda sekondari lakini hawaelewi kitu kutokana na mazingira waliyotoka,” amesema.
Amefafanua kuwa wale wasioelewa kitu baadaye wanaamua kuwa watoro na na wengine mimba za utotoni au wanaishia mitaani,” amesema.
Amesema katika baadhi ya maeneo wazazi wamekuwa wakiwalipa walimu wa kujitolea ili kukabiliana na changamoto hiyo, lakini bado hali si nzuri kwa kuwa hawawezi kulipa walimu kukidhi upungufu uliopo kutokana na hali za kiuchumi walizo nazo.
Kwa upande wake, Mwanahamisi Hassan amesema mbali na upungufu wa walimu, pia, zipo shule kongwe ambazo miundombinu yake ni chakavu na hivyo kuomba Serikali kuzifanyia ukarabati kama ilivyofanya kwenye shule nyingine.
“Ukiangalia shule ya msingi Kigonigoni ilijengwa mwaka 1978, kwa sasa miundombinu yake ya madarasa ni chakavu lakini pia vyoo ni chakavu na havitoshelezi, kwani yapo matundu tisa tu huku wanafunzi wakiwa ni zaidi ya 400,” amesema Mwanahamisi.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya amesema changamoto ya walimu wa shule za msingi ni kubwa hasa katika maeneo ya vijijini.
“Ukiangalia ikama ya walimu, upungufu ni mkubwa sana na shule nyingi bado tunahitaji walimu kwani kuna shule unaweza ukaenda ukakuta kuna walimu wawili, nyingine watatu au wanne,” amesema Mwaipaya.
Ameongeza kuwa: “Niseme tu katika maeneo ambayo mmepita ya Kigonigoni mmeona upungufu ni kweli, lakini jitihada za Serikali ni kuhakikisha kwamba kwa kadri nafasi inapopatikana ajira zinapotoka kwa walimu basi wanaajiriwa ili kukabiliana na changamoto hiyo.”
Mwaipaya amewapongeza walimu waliopo kuwa pamoja na uchache wao, wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
“Pamoja na changamoto hizo bado kwenye taaluma shule zetu zinafanya vizuri ambapo walimu wachache waliopo wanapambana kufanya kazi kwa bidii, kwani changamoto inaweza ikawa kubwa kwa sababu mwalimu mmoja anaweza kuwa na masomo mengi.
“Lakini pia unaweza kukuta changamoto tena za wanafunzi maana ukiangalia utaratibu ule wa uwiano kati ya mwalimu na mwanafunzi kwa darasa la kawaida unakuta mwalimu mmoja wanafunzi 45 au 50 lakini unakuja kukuta darasa moja limefurika wanafunzi hata 100 lakini mwalimu huyo mmoja atoke hapo aende darasa lingine,” amesema Mwaipaya.