Mbeya. Uzalishaji wa ndizi katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya umeshuka mwaka baada ya mazao hayo kushindwa kukomaa kwa wakati kutokana na baridi kali wilayani humo kwenye miezi ya Juni na Julai.
Kutokana na changamoto hiyo, mahitaji ya ndizi yamekuwa makubwa, hali inayosababisha wakulima kuziuza chache zilizopo kwa bei ya juu katika masoko yaliyopo Malawi, Zambia na Botswana kwa nje ya nchi; na mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Iringa, Tunduma mkoani Songwe na Jiji la Mbeya.
Wakulima waliozungumza na Mwananchi wameeleza namna baridi inavyosababisha kupungua kwa uzalishaji wa ndizi na kusababisha kupaa kwa bei ya zao hilo, hasa kwa wanunuzi wa rejareja ambao ni wananchi.
Mkulima na mfanyabiashara wa ndizi kutoka kata ya Kiwira, Debora Ezron amesema kwa msimu huu hali ya uchumi kwao imekuwa ngumu kufuatia mahitaji ya ndizi kuwa makubwa na uzalishaji kuwa chini.
“Unajua changamoto kubwa licha ya baridi, ni ukosefu wa soko la uhakika, hili ni mwiba kwetu endapo lingekuwepo kuna wakati tungeuza kwa faida na kujikwamua kiuchumi,” amesema akisisitiza Serikali iharakishe ujenzi wa soko la kimataifa la ndizi.
Debora ametoa mfano wa mkungu wa ndizi uliokuwa unauzwa Sh8,000 hadi Sh10,000, sasa unauzwa Sh15,000 hadi Sh20,000 tofauti na misimu mingine ambayo uzalishaji unakuwa mkubwa.
Kwa upande wake, mfanyabishara na msafirishaji wa ndizi, Tabu Aloyce amesema msimu huu ndizi zimekuwa za shida, wananunua mkungu mmoja kati ya Sh18, 000 hadi Sh13, 000 kulingana, mbali na gharama za usafirishaji kutoka shambani kwa mkulima.
Akiwa na mtazamo kama huo, mfanyabiashara wa rejareja, Neema Samora amesema wananunua ndizi mbivu sita hadi saba kwa Sh500 na wao wanauza moja Sh200 kulingana na ukubwa.
“Kuna msimu ndizi hiyo hiyo tunauza Sh100 kulingana na namna tunavyonunu sokoni hivyo hivyo ndizi mbichi za kupika tunauza kulingana na tunavyojumlishiwa na wafanyabiashara wanaoziingiza sokoni,” amesema.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Julai 19, 2024, Ofisa Kilimo Wilaya ya Rungwe, Juma Mzara amesema kila mwaka ifikapo Juni hadi Julai, hali ya uzalishaji wa ndizi unakuwa si nzuri kutokana na baridi kali.
“Hata ukiangalia majani ya migomba yanakuwa kama yana ugonjwa kutokana na kiwango kikubwa cha baridi ambacho huathiri na kuyakausha kila kuchapo,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo, mahitaji ya ndizi ni makubwa huku uzalishaji ukiwa chini na kusababisha wafanyabiashara kununua kupandisha bei.
Amesema mbali na changamoto hiyo kwa msimu huu, wastani wa tani 550,000 zimezalishwa huku matarajio kwa msimu ujao yakiwa ni kuzalisha tani 667,000 sambamba na uwepo wa masoko ya uhakika.
Mzara amesema ili wakulima waweze kuwa na uhakika wa masoko na kuongeza tija ya uzalishaji, halmashauri imetenga zaidi ya Sh5.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa la ndizi katika Kata ya Kiwira, eneo la Karasha.
“Tunatarajia kuongeza wigo wa masoko ya ndani na nje na uwepo wa soko hilo utakuwa mwarobaini mkulima kuuza mazao kupitia kwa madalali ambao wamekuwa mwiba kwao,” amesema.