Rombo. Dereva wa bodabodo, Jackson Ngowi (24), mkazi wa Kijiji cha Maharo, Kata ya Makiidi, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, aliyetoweka kwa siku tano, mwili wake umekutwa ukiwa umetelekezwa kwenye moja ya shamba lililopo katika Kijiji cha Ngambeni ukiwa umeharibika.
Kijana huyo anadaiwa kutoweka Julai 14, 2024 baada ya kukodiwa na mtu asiyefahamika, huku wenzake kijiweni kwake anakofanyia kazi wakidhani ni abiria wa kawaida.
Baada ya kuondoka na mteja huyo hakuonekana tena kijiweni hapo wala nyumbani kwao, mpaka mwili wake ulipokutwa jana jioni ukiwa umetelekezwa kwenye shamba hilo.
Taarifa zinadaiwa baada ya kutoonekana nyumbani kwao, jitihada za kumtafuta zilifanyika sambamba na kutoa taarifa Kituo cha Polisi Mkuu.
Hata hivyo, simu zake na pikipiki yake hazijulikani zilipo.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Julai 19, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema baada ya kijana huyo kutoweka nyumbani kwao, familia ilitoa taarifa polisi ambalo lilimsaka kabla mwili wake kuokotwa jana jioni.
“Ni kweli tunafanya uchunguzi wa tukio hili kwa sababu mwanzoni tulipokea taarifa za kupotea kwake, lakini jana tukapata taarifa ya mwili wake kukutwa umetelekezwa shambani ukiwa umeharibika. Sasa tunachunguza kujua kama ni kifo cha kawaida au kimesababishwa na binadamu,” amesema Kamanda Maigwa.
Kamanda Maigwa amesema tayari wamefungua jalada la uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Aidha, amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Huruma wilayani Rombo ukisubiri uchunguzi wa kidakatri kubaini sababu za kifo hicho.
Akizungumzia kupotea kwa kijana huyo, mmoja wa marafiki zake Ngowi ambaye pia ni msemaji wa familia yake, Micky Kinabo amesema Julai 14 kuna abiria alifika kijiweni kwao eneo la Mkuu Kanisani akamkodi.
“Lakini kwa kuwa huwa hatuna kawaida ya kuulizana unaenda wapi baada ya kukodiwa, basi akaondoka,” amesimulia Kinabo.
Lakini baada ya hapo, Kinabo anasema Ngowi hakuonekna tena kijiweni hapo wala nyumbani kwao mpaka maiti yake ilipookotwa shambani jana jioni.
“Tulipoambiwa hapatikani, Jumatatu (Julai 14) madereva bodaboda wote tulianza kumtafuta tukishirikiana na ndugu zake na tulikwenda wote kutoa taarifa polisi na tukasambaza taarifa kwenye makundi yetu yote ya WhatsApp, hospitali lakini hatukufanikiwa kumpata mpaka tulipopata taarifa jana saa 11 jioni kwamba mwili wake umeonekana maeneo ya Ngambeni,” amesema Kinabo.
Kinabo amesema Ngowi atazikwa nyumbani kwao kesho Jumamosi Julai 20, 2024 baada ya taratibu za kipolisi kukamilika.