Arusha. Mahakama ya Rufani nchini imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyopewa Musa Kanyerere, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mama mkwe wake, Helena Hilomeji.
Mahakama hiyo imerudisha jalada la kesi kwenye Mahakama ya Wilaya ya Magu kwa Hakimu mwingine, kwa ajili ya kuhamisha shauri kwenda Mahakama Kuu, baada ya kubaini utaratibu ulikiukwa.
Kwa hatua hiyo, mshtakiwa husomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo, kisha jalada kuhamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya usikilizwaji.
Wakati huohuo, mrufani atasalia kizuizini akisubiri kesi dhidi yake kusikilizwa upya.
Uamuzi huo umetolewa jana Alhamisi Julai 18, 2024 baada ya majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo kubaini kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria ambao ulisababisha mrufani kutotendewa haki na upande wa mashtaka.
Rufaa hiyo ya jinai namba 318/2020 ilisikilizwa na majaji watatu wakiongozwa na Ferdinand Wambali, wengine ni Paul Kihwelo na Abdul-Hakim Amer Issa.
Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza wa Juni 25, 2020.
Awali, Musa alipandishwa kizimbani akikabiliwa na kosa la mauaji ya kukusudia na alihukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Musa alidaiwa Novemba 18, 2014 katika Kijiji cha Sese, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, alimuua mama mkwe wake, Helena, shtaka ambalo alikana kulitenda.
Katika kuthibitisha kosa hilo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watatu ambao waliishawishi mahakama na kumuhukumu adhabu hiyo, ambayo hakuridhishwa nayo akakata rufaa akiwa na sababu nane.
Akiwakilishwa na Wakili Seleman Gilla, mrufani alisema mwenendo wa kesi hiyo ulikuwa na dosari kwani maelezo na nyaraka za sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka hazikusomwa kwa mshtakiwa, hivyo kukiuka masharti ya lazima ya kifungu cha 246(2) na (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Pili, alisema mahakama ya awali ilikosea kisheria katika kumtia hatiani kwa kuzingatia maelezo ya onyo, ambayo hayakuthibitishwa na yalichukuliwa zaidi ya saa nne tangu kukamatwa kwake.
Tatu, kwamba mahakama ya awali ilikosea kisheria kumtia hatiani mrufani kwa kosa aliloshtakiwa nalo wakati upande wa mashtaka haujathibitisha pasipo shaka.
Upande wa mjibu rufaa (Jamhuri) uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Magreth Mwaseba.
Kuhusu hoja ya kwanza, alisema maelezo ya mashahidi na vielelezo vilivyotarajiwa kuwasilishwa katika shauri hilo havijasomwa wakati wa mashauri na hivyo kuwa batili.
Wakili huyo aliiomba Mahakama kufuta shauri hilo kuanzia Oktoba 21, 2016 wakati lilipoanza hadi Juni 25, 2020 hukumu ya ilipotolewa na iamuru kesi isikilizwe upya.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Mwaseba aliunga mkono hoja hiyo ya kwanza ya rufaa na kueleza kuwa rekodi ya kukata rufaa iko wazi kwamba mwenendo wa mashauri haukuwa wa kawaida.
Alidai kuwa moja ya kifungu kilichotumika kufanya uamuzi ni kifungu cha 245 cha CPA badala ya kifungu cha 246 na kuwa kifungu cha 246 (2) ambacho ndio kiini cha ushahidi wa mashahidi wote wa upande wa mashtaka, hakijasomwa.
Wakili aliiomba Mahakama kutumia mamlaka yake chini ya kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa, Sura ya 141 (AJA) kufuta mwenendo wa mashauri ya mahakama hizo za chini kufuta hatia na adhabu hiyo na kuamuru kesi kuanza upya.
Jaji Issa alieleza kuwa suala la uamuzi wao katika rufaa hiyo ni endapo shauri liliendeshwa kwa mujibu wa sheria na kama sivyo nini njia ya kuendelea.
Kwa mujibu wa sheria wakati wa uhamishaji kesi, washtakiwa/mshtakiwa anasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo hatua inayohitimisha uchunguzi wa awali kwenye mahakama ya chini (PI) na jalada kufungwa kisha kuhamishiwa mahakama yenye mamlaka ya kuisikiliza.
Jaji alieleza kifungu cha 246 (2) cha CPA kinaeleza mtuhumiwa atakapofikishwa mbele yake, mahakama ya chini itasoma na kueleza taarifa zilizoletwa dhidi yake au nyaraka zenye kiini cha ushahidi wa mashahidi ambao Mkurugenzi wa Mashtaka anakusudia kuwaita kwenye kesi.
Jaji alieleza baada ya kutii masharti ya vifungu vidogo vya (1) na (2) Mahakama itamwambia mtuhumiwa kwa maneno yafuatayo:
“Sasa umesikia kiini cha ushahidi ambao upande wa mashtaka unakusudia kuuita katika kesi yako, unaweza kuhifadhi utetezi wako na una uhuru wa kusema chochote kuhusiana na shtaka dhidi yako. Chochote utakachosema ama kitaondolewa au kinaweza kutumika kama ushahidi kwenye kesi yako.”
Jaji Issa alieleza kuwa wakirejea katika rufaa hii, rekodi ya Oktoba 21, 2016, haiachi shaka kuwa kulikiukwa kifungu cha 246 (2) na (3) cha CPA.
“Katika hali hiyo, tunakubaliana kabisa na mawakili wa pande zote mbili kwamba kitendo cha mahakama kutotii kifungu hicho,ulikuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria ambao ulisababisha kutotendewa haki kwa mrufani,” alieleza.
Jaji Issa alieleza kwa kuruhusu msingi wa kwanza wa kukata rufaa hawaoni haja ya kuamua sababu ya pili na tatu, hivyo wanaikubali rufaa hiyo.
Jaji Issa alieleza wanatumia kifungu cha 4(2) cha AJA kurekebisha na kubatilisha mashauri ya Mahakama ya Wilaya ya Magu ya Oktoba 16, 2016 na yale ya Mahakama Kuu katika vikao vyake vya jinai na kufuta hatia na hukumu hiyo.