Dar es Salaam. Sekta ya usafiri wa anga nchini huenda ikaathiriwa na hitilafu iliyotokea leo Julai 19, 2024 katika mifumo ya mawasiliano ya Microsoft duniani unahusiana na Falcon Sensor, huku chanzo kikitajwa kuwa ni mchakato wa kuhuisha mifumo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Daniel Malanga, ameeleza athari zilizoletwa na changamoto hiyo ni uwezekano wa kuwepo athari ya safari za ndege, akisema, “usafiri wa anga ni sekta ya kimataifa.”
“Mpaka sasa hakuna abiria au shirika la ndege nchini lililoathirika moja kwa moja, ila inawezekana ikatokea siku zijazo kwa kuwa Tanzania ni sehemu ya usafiri wa anga wa kimataifa.
Aidha, akizungumza na gazeti dada la The Citizen, Malanga ameisema, “Watu wanaowasili Tanzania wanatoka kila pembe ya dunia, ikiwa ni pamoja na nchi zilizoathiriwa moja kwa moja na kukatika kwa mtandao duniani, hii ni pamoja na mashirika ya ndege yenye mikataba ya ndani inayohusisha wasafirishaji kutoka nchi hizi zilizoathirika,” amesema Malanga na kusisitiza Tanzania ni sehemu ya mtandao wa usafiri wa anga duniani.
Malanga hakutaja idadi ya ndege zilizoathiriwa, lakini amesisitiza utegemezi wa Tanzania kwa mashirika ya ndege ya kimataifa.
“Ndani ya nchi, pia tunaathirika kwa sababu mashirika yetu ya ndege ya ndani yanategemea ndege za kimataifa kulisha abiria kutoka njia za ndani au zile zinazohamishwa kutoka safari za kimataifa kwenda nchi za ndani,” amefafanua.
Hata hivyo, kwa upande wa viwanja vya ndege vya Tanzania Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Mussa Mbura ameliambia Mwananchi kuwa mpaka muda huo hakuna athari zilizokuwa zimeonekana na shughuli zinaendelea kama kawaida.
Kwa upande wa mawasiliano, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) Dk Jabiri Bakari amesema wanatambua changamoto hiyo ya mtandao duniani na wanafuatilia kwa karibu suala hilo.
Dk Bakari amesema wameanza kushauriana na wadau wao juu ya hatua za kuchukua, ili zisilete madhara. “Changamoto iliyopo ni kuhusu wanaotumia mfumo wa Microsoft, sio mifumo yote maana wangekuwa wote mazungumzo yasingewezekana, tupo kazini kufuatilia kinachoendelea na kuwashauri wadau wetu wasipate tabu na madhara,” amesema.
Mapema leo imeripotiwa kuwepo hitilafu ya mifumo ya teknolojia ya Microsoft duniani, ikitajwa kuathiri mifumo ya mashirika ya ndege, vyombo vya habari, hospitali na benki kwa asilimia kubwa duniani.
Vyombo vya habari mbalimbali, hususan vya magharibi imeelezwa asilimia 90 ya safari za ndege katika mataifa yaliyoathirika zaidi zimesitishwa.
Baadhi ya maeneo yaliyoripoti kuathirikia zaidi ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Sydney, Shirika la Ndege la United Airlines na Soko la Hisa la Uingereza (LSE).
Taarifa ya BBC imeeleza kuwa mashirika ya utangazaji, benki na hospitali zimeathirika nchini Marekani, Uingereza na Australia.
Microsoft katika taarifa yake imekiri kuwepo na hitilafu kwenye vifaa vinavyotumia Windows.
“Tunafahamu suala linaloathiri vifaa vya Windows kwa sababu ya mchakato wa kuhuisha unaofanywa na mtoa huduma mwingine. Tunatarajia kuja na suluhu,” amesema.