Waziri Ummy: Malalamiko pekee sasa ni ukubwa gharama Muhimbili

Dar es Salaam. Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema gharama kubwa za matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam ndio malalamiko pekee anayopokea kutoka kwa wananchi.

Amesema kwa kiasi kikubwa hospitali hiyo imekuwa na mabadiliko makubwa na hapati malalamiko ya wagonjwa kuzungushwa kupata huduma bali gharama za matibabu ndizo zinalalamikiwa.

“Kwa kweli Muhimbili sipati malalamiko yeyote, nikipata malalamiko ni gharama kubwa, malalamiko kwamba nimezungushwa, nimepigwa danadana sikumbuki,” amesema Waziri Ummy.

Ummy ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 19, 2024 alipotembelea hospitali hiyo na kupokea taarifa ya wagonjwa 28 waliopatiwa huduma kwa msaada wa fedha za Serikali.

Wagonjwa hao ni waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza figo, kuwekewa vifaa maalumu vya usikivu na upandikizaji uloto kwenye mifupa.

Kwa mgonjwa aliyepandikizwa uloto gharama yake ni Sh69 milioni, vifaa vya usikivu Sh45 milioni na upandikizaji figo Sh30 milioni.

Waziri huyo amesema Watanzania wengi wanahitaji huduma bora za matibabu lakini uwezo ni mdogo, hivyo Serikali imekwishalifanyia kazi tatizo hilo kwa kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Hata hivyo, amesema asilimia 80 ya watu wanakata bima ya vifurushi wakiwa tayari wagonjwa, lakini bima ya afya kwa wote itapunguza gharama za michango na ubaguzi katika utoaji huduma.

“Watu watasema Bima ya Afya kwa Wote itaanza lini, tayari tumeshapitisha sheria, tunakamilisha kanuni na tunatoa elimu na hamasa kwenye jamii ili tukitangaza watu wote wanakwenda kujiunga,” amesema.

Ummy amesema kwa sasa Serikali inaimarisha huduma za kibingwa na ubobebezi na mwaka huu tayari Sh6 bilioni zimetengwa kuimarisha huduma hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema kati ya Sh5 bilioni zilizotolewa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kuimarisha huduma za kibingwa nchini, hospitali hiyo imepatiwa mgao wa Sh2.6 bilioni kutoa huduma kwa wananchi.

“Tayari tumeshatoa huduma kwa watu 28 wakiwemo wagonjwa sita wa figo, watoto 16 kupandikizwa vifa vya usikivu na watu sita kupandikizwa uloto,”amesema.

Kuhusu upandikizaji wa uloto, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu Muhimbili Dk Mbonea Yonazi amezungumzia sababu kubwa ya mtu kupandikizwa uloto:

“Dalili za mtu mwenye tatizo la uloto ni upungufu wa uwekundu wa damu, kuchoka kupita kiasi, kizunguzungu, kupata homa na damu kushindwa kuganda,” amesema.

Ametaja aina ya watu wanaopatiwa matibabu hayo kuwa ni mwenye saratani ya damu au selimundu.

Kolumbia Pius, mama aliyepandikizwa uloto hospitalini hapo amesema kabla ya kupandikizwa alifanyiwa upasuaji kwenye Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kuondolewa uvimbe mgongoni.

Amesema baada ya kuondolewa uvimbe huo aliwekewa vyumba mgongoni na baada ya muda alivyopima afya yake aligundulika kuwa na saratani ya damu.

“Baada ya kugundulika kuwa na saratani ndipo nikaelezwa kuwa nitafanyiwa upasuaji wa kupandikiza uloto na sasa afya yangu imeimarika,”amesema.

Naye Mkuu wa Idara ya Pua, Koo na Masikio (MNH) Dk Aslam Nkya amesema tatizo la usikivu kwa watoto hutokana na kuzaliwa au mazingira.

Amesema ili kuwepo kwa ufanisi wa matibabu ni muhimu wazazi wenye watoto wanaopitia changamoto ya usikivu wapelekwe hospitali mapema.

“Kwa watoto watakaozaliwa hapa, tuna kitengo maalumu kwa ajil ya kutambua kama wana shida ya usikivu, matibabu ni rahisi ikiwa mtoto ataletwa hospitali mwaka wa pili baada ya kuzaliwa,” amesema.

Kuhusu upandikizaji figo, Yusta Tarimo amesema mwaka 2016 alianza kuugua figo kwa mashavu kuvimba na 2017 alipimwa na kuambiwa anasumbuliwa na tatizo hilo, hivyo aanze matibabu ya kusafisha damu.

“Baada ya kusafisha figo, nilishauriwa nifanyiwe upandikizaji na mwaka 2018 mama yangu alichangia figo na sasa naendela vizuri, nina watoto wawili, mmoja nilimpata 2021 na mwingine 2024,” amesema.

Related Posts