Anayeuguliwa na mtoto adai kukimbiwa na mume, atolewa vyombo nje kisa kodi

Morogoro. Evelina Sales, mkazi wa Lukobe, Manispaa ya Morogoro, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kukimbiwa na mumewe akidai ni kutokana na mtoto wao kuugua muda mrefu.

Mbali na kukimbiwa na mume, mama huyo amesema wakati amelazwa na mwanawe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, mwenye nyumba wake alimtolea vyombo nje kwa sababu alikuwa hajamlipa kodi kwa muda mrefu.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Julai 19, 2024, Evelina ambaye sasa anaishi kwenye pagale alilofadhiliwa na raia mwema, amesema, “baada ya kujifungua mwanangu katika Hospitali ya Rufaa Morogoro na kuruhusiwa kwenda nyumbani, tulibaini hana njia ya kutolea haja kubwa, tukalazimika kurudi hospitali, wakatupa rufaa kwenda Hospitali ya Muhimbili. Kabla ya kwenda nikampigia simu mume wangu ili nimwambie, hakupokea simu mpaka leo sijui alipo,” anasimulia mama huyo.

Evelina amesema licha ya kuruhusiwa kutoka hospitali, aliambiwa anadaiwa Sh800, 000 za matibabu alizoambiwa atazilipa atakapomrudisha tena mwanawe hospitali.

Akisimulia matibabu aliyoyapata hospitali ya Rufaa Morogoro kabla ya kuhamishiwa Muhimbili, Evelina amesema mwanawe alifanyiwa upasuaji mdogo wa kumwezesha kutoa haja kubwa kupitia ubavuni. “Walisema pale watampa tiba ya upasuaji mdogo tu ili wamwezeshe kutoa uchafu kupitia tundu la ubavuni tu,” amesema.

Anasema alipofika Muhimbili, aliambiwa mwanawe anatakiwa afanyiwe upasuaji mkubwa na gharama yake ni Sh2 milioni. “Ila niliambiwa kama nitatumia bima nitalipa Sh1.5 milioni, nikawaambi sina hizi hela na wakati huo nilikuwa nadaiwa tena hela nyingine ya matibabu Sh800,000, basi wakaniruhusu ila wakasema nitakapoenda kwa ajili ya upasuaji niende na hela zote, sasa sina ndiyo maana niko hapa na mtoto mpaka leo,” amesema mama huyo mwenye watoto wawili. Hata hivyo, mtoto huyo anatakiwa kufanyiwa operesheni mbili, moja ya kurekebisha eneo analotolea haja kubwa sasa na ya pili ni ya kuchana ili kupata njia ya haja kubwa na kila upasuaji unagharimu Sh2 milioni. “Kwa hiyo natakiwa nilipe jumla ya Sh4 milioni kwa upasuaji wote,” amesema.

Evelina amesema baada ya kurudi kutoka Muhimbili alikokuwa amekaa kwa miezi mitatu na alikuwa akidaiwa kodi ya miezi saba ambayo ni Sh70,000. Anasema alidhani mumewe alikuwa akilipa kodi licha ya kuwa alimtelekeza tayari, kumbe haikuwa hivyo.

“Mume wangu alikimbia bila kulipa kodi, yule mwenye nyumba akatufukuza, katika kuzungumza na watu nikawaeleza hali ninayopitia, akatokea msamaria mwema akaniambia yeye anayo nyumba yake haijakamilika akanipa niishi hapa lakini niwe napafanyia usafi tu,” amesema Evelina.

Evelina anasema hali ya mwanawe inazidi kudhoofu siku hadi siku kutokana na kukosa matibabu. Anasema eneo alilofanyiwa upasuaji linatoa usaha lakini pia anaendelea kuvimba.

“Naiomba Serikali na wasamaria wema wajitokeze kunusuru maisha ya mwanangu wanisaidie aweze kupata matibabu waliyoyasema madaktari, mimi sina uwezo wa kupata hizo hela za kumtibu hali ya kidonda inazidi kuwa mbaya, kinatoa harufu na usaha mwingi,” amesema Evelina.

Polisi Kata wa Lukobe, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Zuwena Mwita, ameguswa na maisha ya familia hiyo baada ya Evelina kumfuata akimwomba msaada wa kuwasiliana na jamii ili apate msaada wa matibabu kwa mwanawe.

“Nilikuwa kwenye harakati zangu za kutoa elimu kwa jamii, ndipo mama huyu akanifuata na kunieleza changamoto anayopitia mtoto wake,” amesema.

Anasema alifika nyumbani kwake na kumuona mtoto huyo, aliyesema anahitaji msaada huku akitoa rai kwa watu wenye mapenzi mema wajitokeze kumsaidia mtoto huyo apate matibabu na mahitaji muhimu ya kila siku.

“Kiukweli mtoto anahitaji matibabu ya haraka, nilichofanya niliomba wadau angalau apate kwanza mahitaji muhimu, naombeni Watanzania mumsaidie angalau na yeye aje atimize ndoto zake,” amesema Mwita.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Tecra John, ameweka wazi kuwa wanafahamu changamoto zinazomkabili Evelina na wamejaribu kumsaidia kwa jitihada kadhaa, lakini kutokana na hali ngumu ya maisha, hawakufanikiwa kutoa msaada wa kutosha.

Mwenyekiti huyo amesema msaada mkubwa anaohitaji Evelina kwa sasa ni matibabu ya mtoto wake ambaye ameugua kwa muda mrefu sasa kutokana na kukosa fedha za matibabu.

“Kuhusu makazi kwa sasa amepata msamaria mwema amempa nyumba ya kuishi, hata hivyo suala la haraka ni kutibiwa kwa mtoto,” amesema Tecra.

Related Posts