Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kurekebisha mifumo ili kuwe na Tume Huru ya Uchaguzi na Katiba mpya itamkayolinda na kutetea masilahi ya Watanzania wenye hali duni, wakiwemo wafanyabiashara wadogo na wakulima.
Amesema hayo alipohutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana Aprili 24, 2024 katika stendi ya zamani ya mabasi mjini Bariadi mara baada ya kufanyika kwa maandamano amani.
Mbowe amesema wanaishinikiza Serikali kuweka mifumo huru iyakayotoa haki na usawa kwa wote na kukidhi matakwa ya Watanzania wanaotaka mabadiliko.
Mbowe amesema bado kuna mifumo mibovu na kandamizi inayonyima haki na uhuru wa wananchi na kupoka haki hizo kwa Watanzania wanyonge, wasioweza kupaza sauti zao.
“Sisi kama Chadema tunaitaka Serikali kurekebisha mifumo kandamizi kwa wananchi ambao ndio walipa kodi za Serikali, lakini Serikali hiyo iliyo chini ya Rais Samia haitaki mabadiliko yatakayoleta haki na usawa kwa Watanzania,” amesema.
Amesema katika maandamano wanayofanya katika mikoa mbalimbali wanatembea umbali mrefu bila kuwepo kwa athari kwa wananchi wala mali zao na hivyo akawataka Polisi kuwalinda wananchi na si kuwatishia kwa nafasi walizonazo.
“Askari wanapaswa kutambua kuwa wao ni walinzi wa wananchi ili waishi kwa amani na wanapaswa kutambua uzito wa kazi yao na wasirudi nyuma tena kuanza kutumika kunyima haki za kikatiba,” amesema.
Ameongeza kuwa utakapofikia wakati wa kufanya uchaguzi, watambue uzito wa nafasi zao kwa Watanzania na wasitumike kama ilivyokuwa katika uongozi wa Serikali uliyopita wa Hayati John Magufuli.
Akizungumza katika mkutano huo, kada wa chama hicho, Mdude Nyagali amesema Watanzania wanalia kwa sababu ubovu wa Katiba hauwezi kurekebishika.
“Tanzania ukiwa mkulima au mfugaji haki zako hazitambuliki, hivyo tunataka kurejeshwa kwa mchakato wa Katiba mpya ambayo kupitia hiyo italinda masilahi ya mkulima wa hali ya chini na mfugaji,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Chadema Kanda ya Serengeti, Gimbi Masaba amesema chama hicho katika uchaguzi ujao kisimamie kuhakikisha kinapata wagombea watakaolinda na kutetea masilahi ya wananchi.
“Chaguzi nyingi zilizofanyika chini ya chama tawala zimewanyima haki wananchi kupata haki zao na kusimamia masilahi ya Taifa,” amesema.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Mussa Onesmo amekosoa mpango wa Serikali wa kuwahamisha Wafanyabiashara Bariadi na kuwapeleka nje ya mji, akisema unawapa hasara ya kusafirisha mizigo yao.
“Kuwatoa wafanyabiashara katika eneo wanalotumia kuendesha biashara zao na kulisha familia ni kukiuka Katiba ya nchi na kuminya haki na masilahi ya Watanzania,” amesema.
Akiunga mkono hilo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Bariadi, Johnston Rwezibuka amesema hatua hiyo itarudisha nyuma mitaji yao na kiwafanya wayumbe kimaisha kwa kuwa wamepelekwa mahali pasipokuwa na wateja.