Geita. Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, amesema hajaridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji katika miji 28 baada ya kubaini kuwa ni asilimia 18 pekee ya kazi imekamilika. Akizungumza leo Jumamosi Julai 20, 2024, baada ya kutembelea mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Afcons ya India, naibu waziri huyo amesema hadi sasa utekelezaji hauridhishi na amewataka wafanye kazi usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea.
Mradi huo unajengwa kwa gharama ya Sh124 bilioni, fedha ambazo ni za mkopo nafuu kutoka Serikali ya India, na unatarajiwa kuwanufaisha wakazi zaidi ya 361,000 wa kata 13 za Mji wa Geita na wengine kutoka vijiji 19 vya Halmashauri ya Wilaya hiyo.
“Mradi hadi sasa una asilimia 18 lakini muda uliotumika ni asilimia 45. Mradi ulianza Aprili 2023 na hadi sasa ni miezi 15 imepita kati ya miezi 32 ya mradi. Siwezi kusema nimeridhishwa na utekelezaji, lazima kazi zaidi ifanyike. Nguvu kazi inapaswa kuongezwa ili kufidia muda uliopotezwa,” amesema Mathew.
Kutokana na kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji, Naibu Waziri Mathew ametoa maelekezo ya nini kifanyike ili kukomboa muda uliopotea.
Moja ya maelekezo hayo ni mkandarasi kutoa mpango kazi mpya utakaoonesha namna kazi zitakavyofanyika ili kuokoa muda.
Pia amemtaka mkandarasi kuongeza idadi ya watumishi wakiwemo mafundi, wahandisi, na vibarua na kuagiza kazi zifanyike kwa saa 24. Aidha, ameagiza nguvu kazi itakayoongezwa ipewe mikataba ili kukidhi masharti ya kisheria kwenye shughuli za ukandarasi.
Pia amewataka wananchi ambao mradi unapita kwenye maeneo yao, kutunza vyanzo vya maji na kulinda miundombinu inayojengwa kwenye maeneo yao.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Geita (Geuwasa), Frank Changawa, amesema maeneo ambayo bado utekelezaji uko chini ni pamoja na eneo la kichoteo cha maji (chanzo) kinachotoka Ziwa Victoria.
Eneo jingine ni ujenzi wa mtambo wa kutibu maji unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 45 za maji kwa siku.
Amesema maeneo hayo bado yako chini kutokana na usanifu wa mwisho kutokamilika. “Mradi ulichelewa kutokana na kubadilisha eneo la mtambo wa kutibu maji.
Tumeyapokea maagizo ya Naibu Waziri na tutayasimamia kuhakikisha utekelezaji wa maagizo unafanyika, ikiwemo mpango kazi mpya wa utekelezaji wanaotakiwa kuukabidhi kabla ya Julai 30,” amesema Changawa.
Diwani wa Senga, Thomas Temba, amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha wananchi kupata maji safi na salama na itapunguza magonjwa ya tumbo kama kuhara na kutapika damu yanayosababishwa na maji yasiyo salama.