PAMOJA na hatua nyingi za maendeleo zilizopigwa kwenye soka kama taifa, lakini bado mpira wetu unanogeshwa na porojo nyingi. Bado mpira unachezwa sana mdomoni kuliko hata uwanjani. Mpira wetu una siasa nyingi.
Haji Manara ni msemaji wa Klabu ya Yanga ambaye alikuwa kifungoni. Haji ni muasisi wa usemaji wa majigambo. Amepata umaarufu mkubwa kwa sababu ya propaganda zake kwenye mpira. Zamani ilikuwa ni jambo la wachezaji wa Simba kwenda Yanga, lakini yeye imekuwa ni tofauti.
Haji ni kiongozi na shabiki wa Simba aliyepokewa Yanga. Sio jambo la kawaida, lakini ndiyo uhalisia. Mmejipanga kwa ujio wake mpya? Kwa Haji mdomoni hajawahi kuishiwa maneno.
Kuna muda unakutana na mtu asiyejua kabisa soka, lakini anamkubali huyu binadamu. Kama mdomo ungekuwa unaipa timu pointi tatu kila mechi, Yanga tayari ingekuwa bingwa baada ya kutangazwa kurudi kwa Haji.
Moja kati ya silaha za Haji ni kujua soka. Ni mtangazaji na mwandishi wa michezo mwenye historia na kumbukumbu lukuki za soka letu. Ni mwandishi mkongwe. Alizaliwa kwenye mpira, amekua kwenye mpira na anaishi kwenye mpira. Ni kama Lionel Messi mdomoni. Ni kama Cristiano Ronaldo anayetumia mdomo. Kuna muda anaonekana kuwa na kelele nyingi, lakini haiondoi ukweli kuwa mpira wetu bado unahitaji kelele zake. Watu wanapenda. Watu wanahamasika.
Haji amekosekana miaka miwili kwa sababu ya kufungiwa na mamlaka za soka nchini kutojihusisha na soka baada ya kumkosea adabu rais wa TFF, Wallace Karia. Hakuna kingine. Maandiko yanasema tuwatii watu wenye mamlaka. Nadhani yeye andiko hilo hakuwahi kulielewa. Kuna muda Haji alitaka kuaminisha mashabiki kwamba ni mkubwa sana.
Kuna muda nahisi aliamini kwamba hakuna wa kumfanya chochote kwenye mpira wetu. Mambo yalikuwa tofauti. Alipigwa kifungo cha miaka miwili na hakufanya lolote. Yaliyotokea yametokea, tugange yajayo.
Bado naamini mpira wetu unamhitaji sana Haji. Watu wetu wa mpira bado wanahitaji kuhamasishwa kwenda uwanjani, kununua jezi na kujiunga ili wawe wanachama. Mtu kama Haji uwezo wake ni mkubwa sana eneo hilo. Wachezaji wetu pia wanahitaji mtu wa kuwaongezea thamani ya ukubwa. Haji anajua sana kucheza na eneo hilo. Ukubwa wa Haji na ushawishi wake utaongeza pia nguvu kwenye mitandao ya kijamii.
Bila Shaka yotote hakuna mchezaji wala kiongozi wa mpira yeyote nchini kwa sasa mwenye ushawishi mtandaoni na idadi kubwa ya wafuasi kumzidi Haji.
Haji ana wafuasi zaidi ya milioni tano kwenye mtandao wa Instagram. Ni wengi kuliko wafuasi wa klabu yake. Ni wengi kuliko wafuasi wa mchezaji yeyote hapa nchini.
Kwa dunia ya leo hilo siyo jambo la kuchukuliwa poa. Amerejea mtu mwenye nguvu. Amerejea mtu mwenye ushawishi mkubwa. Amerejea mtu mwenye maneno wakati mwingine ya kukera kuliko mwingine yeyote kwenye mpira wetu. Ni muda wa kujipanga sawa sawa na mdomo wake. Ni muda wa kupata burudani na karaha zake.
Miaka miwili iliyopita kuna kazi kubwa imefanywa na Ahmed Ally, Ally Kamwe, Zaka Zakazi na Hasheem Ibwe kwa uchache. Wamepiga kazi sana. Hawa ni vijana wa kidijitali. Kuna upekee wa Haji kwenye kuusemea mpira wetu, lakini haiondoi ukweli kuwa Ahmed Ally pale Simba nafasi ameitendea haki. Pale Yanga, Kamwe amekuwa na mwanzo mzuri. Amepiga kazi kubwa. Tayari ameiva kuisemea timu. Zakazi na Ibwe pale Azam FC kuna kazi nzuri wameifanya. Huenda kwenye kizazi hiki cha wasemaji, Haji ameasisi nafasi nyingi ambazo vijana wa sasa wanapita.
Haji ameongeza sana thamani ya nafasi hii muhimu kwenye kuleta taarifa. Mpira wetu bado unahitaji sana watu aina yake. Yanga wanaelekea kutambulisha jezi na utambulisho wa wachezaji Siku ya Wananchi. Bila shaka yoyote Haji ni gwiji pia kwenye shughuli hizo.
Kuna muda amekuwa kama mbeba mabomu kwenye klabu. Klabu inapopitia wakati mgumu amekuwa akichaluliwa nchi nzima. Amekuwa akibeba kejeli nyingi pindi timu inapofanya vibaya. Kama binadamu amekuwa pia na changamoto ya jazba na wakati mwingine mikwaruzano ya hapa na pale.
Hata hivyo urejeo wake nadhani utakuja na tofauti kubwa. Heshima kwa watu wote itarejea. Heshima kwa viongozi wa mpira itarejea na mahusiano mema atakuja ameyaboresha. Najua ni fundi wa kucheza na maneno, lakini heshima inapaswa kuwa mbele. Hakuna mkubwa kuliko mpira wetu. Akirudi na njia ileile kuna namna anaweza kuangukia tena pua.
Hapa Yanga wamelamba dume. Haji anakuja kuwaongezea nguvu kubwa sana mtandaoni. Anakuja kuleta hamasa kubwa sana. Tofauti kubwa ya Haji na wasemaji wengine ni kuujua mpira nje na ndani ya uwanja. Huku hakamatiki. Kuna watu hawajui mpira, lakini wanafurahia kumsikiliza Haji. Utani unanogesha soka letu, lakini asiwakosee watu. Kitendo cha kumfungia kwa miaka miwili ilikuwa ni kufikisha ujumbe pia kuwa hakuna mtu mkubwa kuliko mpira. Najua hakuna pengo lisilozibika, lakini mpira wetu ulimmisi mtu kama Haji. Ana mbwembwe zake za kipekee. Kuna mtu unahitaji kumsikiliza tu. Mpira wetu unazidi kuongezeka thamani kila kukicha kuanzia kwa wachezaji wanaosajiliwa hadi makocha. Udhamnini wa taasisi za fedha ni ishara kuwa tunaaaminika kwa sasa. Tuusemee kwa kiasi. Tusikosee watu. Tusiharibu chapa za biashara za watu. Mpira wetu kwa sasa unashawishi wachezaji kila kona ya Afrika. Mpira kwa sasa ni kiwanda kikubwa cha ajira na mkate wa kila siku.
Watu kama Haji tunawahitaji kuendelea kuukuza mpira. Tunahitaji kuukuza mpira bila kumbomoa mtu mwingine yeyote. Karibu sana Haji, binafsi nilimisi mbwembwe zako. Vijana wengi wa kizazi hiki kuna namna wanajitafuta kwenye njia za Haji, lakini yote ni kwa nia njema kuusogeza mpira mbele. Bado wapiga maneno kama Haji tunawahitaji sana kwenye mpira. Bado propaganda zina nafasi kubwa kwenye kuleta hamasa kwenye mpira.