TANZANIA KUNUFAIKA NA MAFUNZO NCHINI INDIA, DKT. TULIA NA SPIKA INDIA WAJADILI

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, akimpatia zawadi ya ngao yenye picha ya jengo la Bunge la Tanzania Spika wa Bunge la India, Mhe. Om Birla wakati alipomtembelea Ofisini kwake Jijini New Delh nchini India.

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (wa kwanza kulia) akiwa katika kikao cha majadiliano na Spika wa Bunge la India, Mhe. Om Birla (wa kwanza kushoto) katika Ofisi za Bunge hilo zilizopo Jijini New Delh leo tarehe 23 Julai, 2024.

*TANZANIA KUNUFAIKA NA MAFUNZO NCHINI INDIA

BUNGE la India limeahidi kutoa fursa zaidi za mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa umma kupitia Taasisi yake ya Utafiti na Mafunzo ya Kidemokrasia (PRIDE) inayoendeshwa na Bunge hilo.

Ahadi hiyo imetolewa leo tarehe 23 Julai, 2024 na Spika wa Bunge la India (Lok Sabha), Mhe. Om Birla wakati wa mazungumzo yake na Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson katika Ofisi za Bunge hilo Jijini New Delhi.

Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Mhe. Birla amemuelezea Dkt. Tulia kuhusu maboresho yaliyofanywa na Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya ufadhili kwa Watumishi wa umma kutoka nchini mbalimbali Duniani hususani Wabunge na Watumishi wa Mabunge ya nchi hizo.

Vilevile, Mhe. Birla ametoa kipaumbele mahususi kwa Watumishi wa Tanzania kwa kuzingatia urafiki, historia na uhusiano uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na India. Aidha, kwa kutambua pia nafasi ya Dkt. Tulia kuwa Rais wa IPU, ameahidi kupitia PRIDE kushirikiana na IPU kuandaa mafunzo kwa Watumishi na Wabunge Wanachama wa Umoja huo.

Sambamba na hilo, Maspika hao wamezipongeza Serikali zao kwa kuendelea kuimairisha uhusiano wenye kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya Nchi hizo.

“Ushirikiano baina ya Serikali zetu umeimarika zaidi baada ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya mwaka jana imeongeza wigo wa ushirikiano na ndugu zetu wa India. Wajibu wa Mabunge yetu ni kushirikina kwa kuzisimamia na kuzishauri vyema Serikali zetu kutekeleza mikataba hiyo kwa manufaa ya Wananchi wetu”. Amesema Dkt. Tulia

Aidha, Dkt. Tulia ametumia fursa hiyo kulishukuru Bunge la India kwa kumuunga mkono wakati wa kampeni za Uchaguzi wa Urais wa IPU pamoja na Bunge hilo kuendelea kusimamia misingi ya demokrasia, utawala bora na kuongeza idadi ya Wabunge wanawake na makundi maalum katika Bunge hilo.

Related Posts