Ditto akwaa kisiki kesi dhidi ya DStv, afunguka

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa hukumu ya kesi ya madai ya mwanamuziki Lameck Ditto dhidi ya Kampuni ya Multchoice Tanzania Limited maarufu DStv, uamuzi ambao haujaacha kicheko kwa mlalamikaji.

Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bwakeya alifungua kesi ya madai mahakamani hapo mwaka 2020 akiiomba iamuru DStv imlipe fidia ya Sh6 bilioni kwa kutumia wimbo  wa Nchi Yangu aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake wakati wa kampeni za  Fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Pia,  aliiomba Mahakama iamuru alipwe Sh200 milioni kutokana na madhara ya jumla sanjari na malipo ya riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.

Hukumu hiyo iliyosainiwa na jaji mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi ambaye hakuwepo mahakamani ilisomwa na naibu msajili wa Mahakama hiyo, Mery Moyo leo Julai 23, 2024, akisema wimbo uliotumiwa na DStv sio halisi ambao Ditto ndiye mmiliki.

Kabla ya kusoma hukumu hiyo, iliyokuwa na kurasa kumi, Moyo amesema imetolewa na Jaji Maghimbi na yeye amepewa kuisoma huku akianza kwa kueleza katika uumbaji, Mungu ametoa karama mbalimbali ambazo ndiyo chanzo cha kipato na mali.

Moyo amefafanua maana ya haki miliki akisema ni neno la kisheria linalotumika kutafsiri haki ya anayetengeneza kazi fulani akizichanganua kazi hizo ikiwamo ya muziki.

Amesema  hakimiliki inatunza kazi ya asili ambayo imetengenezwa.

Katika hukumu hiyo alizitaja nafuu ambazo Ditto aliziomba katika shauri hilo na kubainisha kwamba, jitihada za kuwasuluhisha kwa sheria ya mwenendo wa madai hazikuweza kufanikiwa.

Ametaja hoja tano zilizokubalika katika shauri hilo ambazo ya kwanza ni je, mdai (Ditto) ni miliki wa wimbo wa Nchi Yangu.

Hoja ya pili kama Ditto ndiye mmiliki, je mdaiwa alitumia wimbo huo?

Hoja ya tatu ni je wimbo huo ndio ambao mdai amesema ni wake?.

Hoja ya nne mdaiwa kuutumia wimbo wa mdai unaunda kutotendewa haki kwa mdai na hoja ya tano ni nafuu gani ambazo pande zote zinastahili.

Katika hukumu hiyo amesema, hoja ya kwanza haikupaswa kujadiliwa kwa sababu hakukuwa na ubishani wa hakimiliki ya wimbo huo ambao una hakimiliki ya Ditto tangu m mwaka 2019.

“Hoja zilizobaki za msingi za kujadiliwa ni hoja ya pili hadi ya tano,” amesema Moyo akifafanua kuhusu hoja hizo kisha akaeleza kwamba, wimbo uliotumiwa na DStv wa Nchi yangu sio wimbo halisi  wa Ditto na kuongeza kwamba ule uliotumia ulikuwa maalumu wa kampeni ya kuhamasisha amani na upendo.

Nje ya Mahakama, Ditto amesema hajaridhishwa na hukumu hiyo akibainisha kukaa na wanasheria kuona nini wafanye.

“Nimepokea hukumu, ingawa sijaridhika nayo, inafahamika popote haki miliki ni mwenye orijino. Kwenye hukumu Mahakama haijakataa kama mimi sio mmiliki wa wimbo wa nchi yangu, lakini inasema DStv haikutumia wimbo original  ambao ni wangu, imetumia version  ya pili, je mwenye wimbo huo ni nani?,” amehoji Ditto kwa uchungu.

Amesema hajaridhika na hukumu hiyo na ataona namna ya kufanya baada ya kuzungumza na wanasheria wake ili akate rufaa.

Mwanasheria wa DStv, Simon Lyimo amegoma kuzungumza hukumu hiyo huku wa Ditto, Samson Lukumay akieleza kwamba wamepokea uamuzi wa Mahakama na watakaa na mteja wao kuona utaratibu wa kukata rufaa.

Katika kesi hiyo, Ditto alipeleka mashahidi watano,  na DStv ilikuwa na mashahidi wawili, Astrid Mapunda na Johnson Mshana wakiongozwa na mawakili, Simon Lyimo na Thomas Mathias.

Upande wa Ditto, baadhi ya mashahidi wake walikuwa ni produzya wa wimbo huo, Emmanuel Maungu (Emma the boy), meneja wake,  Rodney Rugambo na Angela Karashani wakiongozwa na mawikili, Ally Hamza na Elizabeth Mlemeta na Lukumay.

Related Posts