Aliyeipeleka Azam FC colombia ana sehemu yake mbinguni

Ilianzia dirisha dogo la msimu uliopita pale Azam FC walipomtambulisha Franklin Navarro, kiungo wa ushambuliaji kutoka Colombia.

Navarro hakutambulishwa tu kwa jezi bali mechi ya Kombe la Mapinduzi pale alipoingia dakika za mwisho dhidi ya Chipukizi FC ya Zanzibar.

Alipogusa mpira wa kwanza tu kila mtu uwanjani na hata aliyeangalia mechi ile kwenye runinga, alijisemea moyoni Azam FC imepata mchezaji.

Baadaye akaja Yeison Fuentes Mendoza, ambaye baada ya picha za utambulisho, akaonekana kwenye mchezo dhidi ya Simba SC jijini Mwanza.

Tanzania ikapiga muhuri, huyu naye ni mtu, na kwa hawa wacolombia wawili, Azam FC imepata watu.

Bahati mbaya kwa Navarro ambaye mchezo huo dhidi ya Simba aliingia, ukawa mchezo wake pekee rasmi akiwa na Azam FC.

Alipata majeraha ambayo sasa yanamfanya awe hatarini kukatwa.

Hata hivyo, Azam FC ikanogewa na Wacolombia na baada ya msimu ule wakaja wengine wawili ambao muda si mrefu Tanzania itaanza kuwaimba.

Wawili hao ni kiungo Ever Meza na mshambuliaji Jhonier Blanco. Hawa ndio wanaosababisha kumpongeza aliyewapeleka Azam FC Colombia.

Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa sana wa kupiga pasi, kukaba na kuusoma mchezo.

Ana kiwango kikubwa sana cha maarifa ya kuudhibiti mpira. Yaani kwa kifupi ni aina ya viungo wale tunawaita ‘mpe chafu akupe safi’.

Ana uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo na mlinzi wa pembeni. Anajua kucheza mpira wa ufundi na wa kihuni, yaani kukichafua.

Kwa kifupi, Azam FC wamepata kiungo mwenye hadhi ya kuanzia nusu fainali ya ligi ya mabingwa.

Ni mshambuliaji anayejua kufungua na kufunga. Yaani anajua kuzifungua safu za upinzani kwa mikimbio yake, chenga za mpira na chenga za mwili.

Blanco siyo mshambuliaji wa kubaki na mlinzi mmoja, mtalaumiana kambini kwenu. Blanco ni mshambuliaji anayetumia miguu yote miwili kuchezea mpira, siyo kama wale wa mguu mmoja wa kuchezea na mwingine wa kutembelea.

Kama mashabiki wa Azam FC waliumia kumpoteza Prince Dube, basi watashukuru sana baada ya kumuona vizuri huyu kwa sababu watasema Dube aliwachelewesha.

Kocha Yousouph Dabo anasema Wacolombia hawa wana uwezo mkubwa sana wa kucheza mpira, anayohangaika nayo kwao ni kupandikiza mbinu zake.

Hadi sasa mambo yanaenda vizuri japo kuna changamoto kubwa sana ya lugha. Wachezaji hawa wanaongea kihispaniola tu, kocha anaongea Kifaransa na Kiingereza ambacho wao hawaelewi hata kidogo.

Hii ndiyo changamoto pekee hadi sasa, hata hivyo soka lina lugha moja na wanajitajidi kuelewana.

Wakati ni hakimu mzuri sana na kwa kesi ya Wacolombia wa Azam, hakimu wakati ataanza kusikiliza kesi kuanzia Agosti 8 pale Uwanja wa Amaan Zanzibar kwenye Ngao ya Jamii ikishuka dimbani kukwaruzana na Coastal Union ya Tanga, timu inayochukia zaidi kufungwa na Azam FC kuliko kukosa Kombe.

Baada ya Ngao ya Jamii na mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania itaanza kuwazungumzia wachezaji hawa kwa heshima ya hali ya juu sana.

Wakati huo ukifika ndipo aliyewaonyesha Azam njia ya Colombia ataanza kupata thawabu zake zitakazompatia kiwanja chake mbinguni.

Related Posts