Mtaa wa Kisiwani Tabata kupata shule ya msingi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga Sh milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi katika Mtaa wa Kisiwani uliopo Kata ya Tabata.

Kujengwa kwa shule hiyo kutaiwezesha Kata ya Tabata kuwa na shule saba za msingi kati ya mitaa minane iliyopo.

Akizungumza Julai 22,2024 wakati wa mkutano wa hadhara uliohitishwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli na kufanyika katika kata hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jamary Satura, amesema wanatarajia shule hiyo ianze kuchukua wanafunzi Januari mwakani.

Satura alikuwa akizungumza kwa njia ya simu katika mkutano huo baada ya kutakiwa na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Ojambi Masaburi, kujibu hoja za wananchi waliotaka kujua kuhusu ujenzi wa shule hiyo.

“Tunatambua changamoto walizonazo wananchi katika Mtaa wa Kisiwani, katika bajeti ya mwaka 2024/2025 tumetenga Sh milioni 200 kwa ajili ya kuwajengea shule ya msingi, tunasubiri mifumo ifunguliwe mwezi wa nane ujenzi uanze. Tunataka Januari mwakani shule ianze kuchukua wanafunzi,” amesema Satura.

Masaburi amesema watahakikisha fedha hizo zinatolewa kwa wakati na kusimamia ujenzi wa shule hiyo ili ikamilike na kuondoa kero kwa wananchi.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amesema watoto wengi wa mtaaa huo wamekuwa wakilazimika kwenda kusoma katika mitaa mingine hali inayowalazimu kutembea umbali mrefu au kutumia gharama kubwa za usafiri.

“Wananchi wa Kisiwani tayari wanacho kiwanja hivyo, tunaomba ujenzi uharakishwe ili watoto wetu wasome karibu na nyumbani, hii itapunguza gharama na umbali waliokuwa wakiutumia kwenda na kurudi shule,” amesema Bonnah.

Kuhusu ujenzi wa Barabara ya Mwananchi Kisiwani hadi Mawenzi pamoja na daraja, Mhandisi kutoka Tarura Wilaya ya Ilala, Leginald Mashanda, amesema utaanza hivi karibuni kwa kiwango cha zege na utatekelezwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Related Posts