Mbunge alalama uwezo mdogo wa transifoma

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Jesca Kishoa ameitaka Serikali kufunga transifoma zenye ukubwa wa kilovoti 200 hadi 315 ili kukidhi mahitaji ya kuendesha viwanda jimboni Mkalama, mkoani Singida.

Amesema hayo leo Alhamisi Aprili 25, 2024 bungeni Dodoma alipouliza swali la nyongeza kuhusu uwezo mdogo wa transifoma zilizoko jimboni humo zenye ukubwa wa kilovoti 50 na 100.

Kishoa amesema licha ya vijijii vyote jimboni humo kuwa na umeme lakini changamoto ni transifoma zilizofungwa kushindwa kuhimili mahitaji makubwa kwa kuwa wananchi wana viwanda vya alizeti na kuunga vyuma.

Ameitaka Serikali kuona umuhimu wa kufunga transifoma zenye uwezo zaidi ili kuwawezesha wananchi kupata umeme wa uhakika.

Mbali na hilo ameshauri uwepo umakini katika kutafuta wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini, akisema wengi wamekuwa hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Pia amehoji mipango ya Serikali ili kuepuka makosa ya kupata wakandarai wanaosuasua.

Akijibu maswali ya mbunge huyo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itaongeza ukubwa wa transifoma.

Amesema zitakuwapo za kilovoti 50, 100 na 200 na zitafungwa kulingana na mahitaji ya eneo husika.

“Kuhusu wakandarasi wanaosuasua kwenye miradi, maelekezo ya Serikali ni kwamba, hatutawavumilia. Kupitia taasisi zetu za Tanesco na REA hatutawapatia kazi wakandarasi hao kwenye miradi yetu,” amesema Kapinga.

Katika swali la msingi, Kishoa alitaka kujua ni lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme wa REA kwenye vijiji 20 vilivyobaki wilayani Mkalama.

Naibu Waziri Kapinga amesema jimbo la Mkalama lina vijiji 70 na vyote vimepatiwa umeme, vikiwemo 25 vilivyokuwa katika mradi wa kusambaza umeme awamu ya tatu mzunguko wa pili, uliotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Amesema jimbo hilo lina vitongoji 388 na kati ya hivyo, 176 vimepatiwa umeme.

Katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia REA amesema ilitenga fedha za kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya kila jimbo likiwamo la Mkalama.

Kapinga amasema REA inakamilisha taratibu za kuwapata wakandarasi watakaotekeleza mradi jimboni Mkalama.

Naibu waziri amesema jimbo hilo litabakiwa na vitongoji 197 visivyo na umeme ambavyo vitapatiwa nishati hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha.

Related Posts