Mahakama ya wilaya ya Babati imemhukumu kwenda jela miaka 30 Ramadhan Idd Kipusa mwenye umri wa miaka 19 baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka na kumlawiti binti mwenye miaka 19 ambaye ana ulemavu wa kusikia na kuongea.
Hukumu hiyo imetolewa leo Julai 23, 2024, na Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Babati Martin Masao, huku upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Chema Maswi.
Kesi hiyo namba 5310 ya mwaka 2024 imetolewa hukumu na Hakimu wa Mahakama ya wilaya ya Babati ambapo mshtakiwa anakabiliwa na makosa mawili kubaka na kulawiti.
Hakimu Martin ameieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 6 mwaka huu wakati ambapo mama mzazi wa binti huyo alipokuwa amepeleka maandazi dukani ndipo kijana huyo Idd Juma Kipusa alipokwenda ndani kutekeleza matukio hayo.
Mshtakiwa Idd Juma Kipusa anakabiliwa na kosa la kwanza la kubaka ambalo limeelezwa mahakamani hapa kwamba ni kinyume na kifungu cha 130 kifungu kidogo cha kwanza na kifungu cha pili a , ikisomwa sambamba na kifungu cha 131moja ambacho kinatoa adhabu.
Kosa la pili ni kumlawiti binti huyo ambalo ni kinyume na kifungu cha 154 kifungu kidogo cha kwanza a cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mara baada ya mahakama kujiridhisha na ushadi uliotolewa mahakamani hapo, ndipo mahakama hiyo mbele ya hakimu Martin Massao alipomtia hatiani kijana huyu na kumhukumu kwenda jela miaka 30 kwa kila kosa na kumlipa fidia binti huyo ya shilingi laki tano kwa kila kosa.
Mshtakiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea aliieleza mahakama kuwa hajafanya kosa hilo na mahakama imemuonea, huku Hakimu Masao alieleza mahakama kuwa mshtakiwa anahaki ya kukata rufaa.