Kipa wa Simba SC mama’ke ni Yanga

MAMA mzazi wa kipa wa Simba, Hussein Abel, Mwaija Husein Fadhir amekiri kuwa yeye ni Yanga damu lakini hilo halihusiani na kazin ya mwanae.

Amesema mchezo wa dabi anaiombea sana ushindi chama lake Yanga, lakini iwapo Wekundu watampanga mwanae golini anaomba mchezo uwe sare.

Yanga na Simba zinachuana Jumamosi kwenye mechi ya Ligi Kuu, huku wadau na mashabiki wa soka nchini wakisubiri dabi hiyo kwa hamu kutokana na presha ya mechi hiyo.

Timu hizo kongwe nchini zinakutana ikiwa Yanga ina kumbukumbu ya ushindi wa mabao 5-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza na kufanya mchezo wa Jumamosi kuwa na taswira tofauti.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwaija amesema pamoja na matamanio yake Yanga kushinda, lakini iwapo Simba itampanga mwanaye golini, ataomba mchezo huo uishe kwa sare kwani anatamani kumuona kijana wake akidaka dabi hiyo.

“Mtoto wangu amenikuta mimi ni Yanga, kwahiyo nashindwa kuiacha asili yangu, ila natamani nimuone akidaka hiyo dabi ya Jumamosi na uwezo anao, ikiwa hivyo naomba mechi iwe sare, naamini Yanga itaendeleza makali na wanaoweza kuamua mechi ni kati Joseph Guede, Stephen Aziz Ki na Kenedy Musonda kutokana na rekodi na ubora wao kwa mechi za karibuni,” amesema Mwaija.

Shabiki huyo wa soka hakusita kukiri ugumu wa mchezo huo, akieleza kuwa dabi mara nyingi huwa na upinzani licha ya kwamba Simba imepitia kipindi kigumu ila siyo ya kubezwa.

Amesema yeyote aliyejiandaa vyema anaweza kushinda mchezo huo kutokana na uhitaji wa pointi tatu kwa timu zote ili kujiweka mazingira mazuri.

“Sisi Yanga tunaamini tutashinda, ila tunajua dabi mara zote siyo ya kutabiri haraka, yeyote aliyejiandaa vizuri anaweza kushinda, Simba bado wako vizuri tusiwabeze,” amesema mdau huyo wa soka.

Related Posts