Mwamvua Mwinyi, Pwani
JESHI la Polisi Mkoani Pwani kwa kushirikiana na Maofisa usafirishaji Wilaya ya Kibaha (bodaboda), limezindua zoezi la uvaaji viakisi mwanga katika ili kuwa rasmi na kuepuka kukumbwa na majanga mbalimbali ikiwemo kuporwa vyombo vyao vya moto.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ,Pius Lutumo aliwataka maofisa hao kuhakikisha wanajisajili katika kanzi data ili kutambulika pamoja na vijiwe wanavyofanyia kazi.
Alisema endapo wadau hao watajisajili na kutii sheria za usalama barabarani ajali zitapungua kwa kiasi kikubwa, matukio ya wizi kwa kutumia bodaboda yatakwisha na wahalifu wanaojificha kwa mgongo wa bodaboda watadhibitiwa.
Lutumo aliwakumbusha, madereva waliosajiliwa kwenye kanzi data kutowaazima viakisi mwanga vilivyo na namba za utambulisho kwa wenzao ambao hawajajisajili.
“Mkiazimana wanaweza kufanya matukio ya kihalifu na viakisi mwanga vikatumika kama utambulisho wa watuhumiwa hao kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Nae Katibu wa Chama cha Maofisa Usafirishaji Wilaya ya Kibaha, Mwinyichande Mungi alieleza, watatekeleza zoezi hilo kwa weledi na kuhakikisha kila anayetaka kufanya kazi hiyo anafuata taratibu ikiwemo kujisajili na kupata namba ya utambulisho.
Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Kongowe Saimon Mbelwa aliwataka madereva hao kutambua kazi yao ina mchango mkubwa kwa jamii.