Mtaka awatuliza wafanyabiashara kisa mauaji ya mwenzao

Njombe. Mamia ya wananchi wamejitokeza kwenye maziko ya Godfrey Ndambo (45), aliyekuwa mfanyabiashara maarufu mkoani Njombe.

Kabla ya kufanyika kwa maziko hayo, baadhi ya wafanyabiashara walipanga kufunga maduka kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo ili kulishinikiza Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika wa mauaji hayo.

Hata hivyo, baada ya viongozi wa wafanyabiashara hao kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliwasihi wasifunge maduka, akiahidi Serikali kushughulikia jambo hilo.

Ndambo aliyefariki dunia Julai 21, 2024, wakati akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya baada ya kuvamiwa na majambazi nyumbani kwake, maziko yake yamefanyika leo Jumanne Julai, 23, 2024 Njombe mjini.

Wauaji hao walimpiga Ndambo kichwani na kitu kizito akiwa getini nyumbani kwake kisha kutoweka na  Sh47 milioni alizokuwa amezibeba kwenye gari lake.

Mtaka amesema mkoa umepata simanzi kubwa kutokana na kifo cha Ndambo aliyekuwa mfanyabiashara mwenye mafanikio katika sekta binafsi.

 “Nilipopewa taarifa ya tukio, nilimwambia RPC aende nyumbani aone kama kuna kamera. Nikaambiwa kamera zipo lakini huwa zinawashwa na kuzimwa.”

Mkuu huyo wa mkoa amesema mauaji ya aina hiyo hayafanywi na watu wa mbali, isipokuwa ni watoto, ndugu na marafiki.

Amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe kuchukua simu za wanafamilia na watumishi wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi.

Baadhi ya waombolezaji waliojitokeza kwenye ibada ya mazishi ya aliyekuwa mfanyabiashara, Godfrey Ndambo (45) nyumbani kwake Uzunguni mtaa wa Ramandahi wilayani Njombe.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe, Deo Sanga ameiomba Serikali kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanakamatwa.

“Hatuwezi kuvumilia matukio kama haya kwenye mkoa wetu. Imani yetu ni kwamba ndani ya siku mbili majibu yatapatikana,” amesema Sanga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema katika kipindi kifupi kumekuwa na matukio matano ya mauaji likiwamo la Ndambo.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio hayo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ramandahi, Evaristo Mwimba amesema kuna vijana wanaofanya uhalifu kwenye mtaa huo ambao umri wao ni kati ya miaka 18 na kushuka chini.

“Familia hasa wazazi wajitafakari na wawachunguze watoto wao mienendo yao, lakini sisi tunaoishi pamoja huku mitaani tunajuana, tutajane kama tunahisi fulani ni mhalifu ili tukomeshe haya mambo,” amesema Mwimba.

Mwakilishi wa familia, Meshack Ndambo, amewashukuru wananchi wa Njombe mjini kwa kuacha shughuli zao na kuja kushiriki kwenye maziko ya ndugu yao.

“Ni tukio la kihistoria kuacha kabisa siku ya leo kufanya kazi mmejali kifo cha ndugu yetu. Kwa tendo hilo mmeisemesha Serikali nayo imesikia tunaimani uchunguzi wa mauaji haya utafanyika haraka ili wauaji wakamatwe na hatua zichukuliwe dhidi yao,” amesema Ndambo.

Related Posts