IGP Wambura, RPC Tanga wafunguliwa kesi sakata la Kombo

Tanga. Mawakili tisa wanaomwakilisha kada wa Chadema, Kombo Mbwana wamefungua kesi dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camilius Wambura na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, wakiomba mteja wao aachiliwe huru na alipwe fidia.

Kesi hiyo iliyofikishwa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, leo Jumanne Julai 23, 2024 imeahirishwa na Naibu Msajili B.R. Nyki hadi Julai 26, 2024 baada ya Jaji Hapiness Ndesamburo aliyetakiwa kusikiliza kesi kutokuwepo.

Mawakili waliofungua kesi hiyo ni Peter Madeleka, Mpale Mpoki, John Seka, Boniface Mwabukusi, Peter Madeleka, Paul Kisabo, Hekima Mwasipu, Daimu Halfani, Fulgence Massawe na Ferdinand Makore, wakiwashitaki pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Kwa mujibu wa mawakili hao, wanaomba Mahakama iamuru mteja wao aachiliwe katika kizuizi cha mshitakiwa wa kwanza na wa pili.

Pia, wanaomba bila kuingilia kifungu cha kwanza, Mahakama iamuru washitakiwa wafike mahakamani waeleze kwa nini wanamshikilia mteja wao kinyume cha sheria.

Mawakili hao wanataka Mahakama itoe amri ya kuzuia washitakiwa hao kuendelea kumshikilia mteja wao kwa muda mrefu kinyume cha sheria.

Pia,  wanaiomba Mahakama itoe unafuu wowote kati ya uliotajwa hapo juu kwa jinsi itakavyoona.

Katika kusikilizwa pande mbili, mawakili hao wameiomba Mahakama kutoa amri ya kuwaita mahakamani washitakiwa kueleza kwa nini mteja wao ameshikiliwa na amenyimwa uhuru kinyume cha sheria.

Pia, wameiomba Mahakama kutoa amri kwa washitakiwa kumlipa mteja wao fidia kwa kumshiklia kinyume cha sheria, utaratibu na bila sababu ya msingi.

Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024 baada ya watu wasiojulikana kudaiwa kumteka akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Kwamsala wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Hata hivyo, Julai 14, 2024 Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zacharia Bernard alitangaza kuwa wanamshikilia kwa tuhuma za kutumia vifaa vya kielektroniki na laini za simu za mitandao mbalimbali zisizo na usajili, kutekeleza uhalifu huo kinyume cha sheria za nchi.

Julai 17, 2024 ndugu zake walidai kuwa Kombo alipelekwa Mahakama ya Wilaya ya Tanga kushitakiwa kwa makossa matatu, bila wao kujua na baada ya hapo alipelekwa rumande katika Gereza la Maweni mkoani humo.

Related Posts