Makala| Mfahamu Amani Josiah; kocha kijana anayetamani kufundisha soka la Kimataifa

*Ndiye mwasisi wa Biashara United ya Mara

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

AMANI Josiah ni moja ya majina ya makocha vijana wa Kitanzania yaliyotikisa msimu ulioisha kwenye Ligi ya Championship akiifundisha Biashara United ya Mara ambayo manusura aipandishe kwenda Ligi Kuu kabla yam bio zake kukatishwa na Tabora United kwenye mchezo wa mtoano (playoffs).

Akiiongoza Biashara United msimu uliopita akiwa na wasaidizi wake, Edna Lema na Ivo Mapunda, Kocha Josiah aliiwezesha kumaliza katika nafasi ya nne ikivuna pointi 62 katika mechi 30, ikishinda 19, sare tano na kupoteza sita, huku ikifunga mabao 60 na kuruhusu 21.

Timu hiyo ilikuwa kinara wa mabao katika ligi hiyo ikifuatiwa na Pamba Jiji (54) na Ken Gold (51) huku ikiwa ya nne kwa kushinda mechi nyingi (19) ikizidiwa na Ken Gold (21), Pamba Jiji na Mbeya City zilizoshinda 20 kila mmoja.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Boban Bogere alimaliza wa pili kwa mabao mengi (20) nyuma ya kinara Edgar William wa Ken Gold (21), huku kipa wake, Robert Mapigano akipata cleensheet 10 akiwa wa tatu nyuma ya Castor Mhagama wa Ken Gold (19) na Yusuph Abdul wa TMA (15).

MWANZO WA SAFARI YAKE

Safari yake ya kufundisha mpira wa miguu ilianza kama utani kwa kukusanya watoto mtaani mjini Musoma na kuwanunulia viatu, jezi, mipira na vifaa vingine kisha kuwafundisha mbinu mbalimbali alizokuwa anajifunza baada ya kuwatazama makocha wa nje, Sir Alex Ferguson na Arsene Mwenger.

“Nilianza kugaharmika mwenyewe nikawa nakitumia kwa hawa vijana nione namna ambavyo wanaweza wakatekeleza mawazo yangu na kuyawasilisha kucheza, nikawa nakazana angalau nione vijana wanaweza kucheza vizuri kama kile ninachokitamani kutoka Ulaya,” anasema Josiah

“Baada ya hapo nikapata nafasi ya kufundisha klabu mbalimbali mkoani Mara ikiwemo Town Star, Cargo, Igwe, Kigera zikanipa nafasi ya kuonekana na kwa sababu nilikuwa mshindani wa kweli nikabahatika kuchukua ubingwa wa mkoa wa Mara na timu nne tofauti ikiwemo Town Star, Cargo, Igwe FC na Baruti,”

“Nikajikuta nimetengeneza vijana wengi hapa Mara nikapata nafasi ya kufundisha Polisi Mara ikiwa daraja la nne Musoma tukachukua ubingwa wa wilaya, Mkoa na kucheza Kanda na kuipandisha daraja la kwanza pasipo kupoteza mechi yoyote,” anasema Josiah na kuongeza;

“….hiyo ilikuwa ni moja ya historia yangu nzuri kupandisha timu kutoka ligi ya wilaya mpaka daraja la kwanza bila kupoteza mechi zote (mechi 34 mfululizo). Niliachana nao nikaja kuanzisha timu ya wakongwe (maveterani) ya wafanyabiashara hapa Mara ambao walikuwa wanatoka madukani wanakuja kwenye mazoezi,”

BUM YAZALIWA

“Baadaye nikaleta wazo la kuanzisha Biashara United kuwa na vijana ndani ya hao maveterani, wale wafanyabiashara wakanikubalia tukachukua fomu za kushiriki daraja la nne wale vijana wote waliokuwa Polisi Mara niliowatengeneza wakaja kucheza kwangu,”

“Polisi Mara wakanifuata tukachukua nafasi yao na kuiita Biashara United nikatengeneza benchi la ufundi timu ikapata mafanikio na kwenda Ligi Kuu ikipoteza mechi mbili tu, na kuweka historia ya kuwa na timu ya Ligi Kuu mkoa wa Mara kwa mara ya kwanza,” anasema kocha huyo

“Kwahiyo unaweza kuona historia yangu naweza kusema nilipandisha timu kutoka ligi ya wilaya mpaka Ligi Kuu pasipokusimama kwenye kazi yangu. Baada ya kuipandisha Biashara nikawa meneja kwasababu sikuwa na vigezo vya kuwa kocha mkuu,”

“Msimu wa kwanza nikaondoka nikaenda Pamba kuwa mshauri wa ufundi nikadumu kwa miezi sita, nikaenda Tunduru Korosho ikiwa daraja la nne tukatwaa ubingwa wa mkoa wa Ruvuma, tukatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), napo nikaweka historia ya kuipandisha daraja la pili tukipoteza mechi moja tu dhidi ya Pan African,”

“Msimu wetu wa kwanza Daraja la pili tulifuzu nane bora kwenye fainali hizo tulipoteza mechi moja, ambapo Mbuni na Copco walipanda daraja. Kwahiyo tulicheza mechi takribani 34 tukapoteza mechi nne. Baada ya hapo ndipo msimu uliopita nikarudi Biashara United na kuipeleka timu Playoff (mtoano) kabla ya kufungwa na Tabora United,” anaeleza Josiah

KUFANYA VIZURI CHAMPIONSHIP

Kocha huyo anasema siri ya kufanya vizuri msimu uliopita ni kutengeneza kikosi bora kinachocheza soka la kushambulia bila kumtegemea mfungaji mmoja kwani yeye ni muumini wa soka soka safi na timu kucheza kwa muunganiko na maelewano makubwa.

“Ndiyo maana ilikuwa rahisi sana kwetu tulitengeneza timu ya kushambulia na kumiliki mpira zaidi tukiamini kwamba tukiwa na timu ya namna hiyo tutacheza nyumbani na ugenini na kupata matokeo mazuri na kila nafasi uwanjani ilifunga mabao,” anasema Josiah

KUFUNDISHA KIMATAIFA

Josiah anasema kwa sasa ana leseni ya Diploma B ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na mwezi huu atakwenda kujiendeleza kusoma Diploma A ili aweze kukidhi vigezo vya kufundisha soka nje ya nchi, huku akitamani kuwa kama Rulani Mokwema na Pitso Mosimane wa Afrika Kusini waliotoboa kimataifa.

“Nina taaluma ya uongozi wa mpira wa miguu, makipa, utimamu wa mwili na ufundi kwahiyo kwenye soka nimegusa katika maeneo mengi. Na malengo yangu makubwa natamani niwe kocha mkubwa ambaye nitawakilisha Tanzania,” anasema kocha huyo

“Kwa hapa naiona kazi bado niko nayo ninachokifanya nijiboreshe kwenye utawala kwanza na elimu niwe na vigezo vinavyonitosheleza baada ya hapo ni-push nione ninaweza kuwa miongoni mwa makocha bora kwenye nchi yetu, lakini nawaza zaidi kufundisha nje,” anasema

Josiah anasema kutokana na uwezo alioonyesha msimu uliopita baadhi ya timu za nje zimeanza kuvutiwa naye na kumtafuta lakini anasubiri kumaliza masomo yake ya Diploma A ili akidhi vigezo vya kufundisha kimataifa na kukidhi mahitaji ya soka la kisasa.

MAKOCHA WANAOMVUTIA

Anasema anavutiwa na makocha wengi wazawa akiwemo Ahmad Ally (JKT Tanzania), Malale Hamsini, Mohamed Bares (Mashujaa), Emmanuel Budeba (Mbuni), Ngawina Ngawina (Coastal Union), Maka Mwalwisi, Juma Mgunda, Mohamed Kijuso na Mathias Wandiba.

“Wote ni makocha wanaofanya vizuri, pia kuna kijana anaitwa Mohamed Mrishona maarufu ‘Xavi’ yuko timu ya vijana ya Simba ni kijana anayekuja vizuri sana. Kiujumla tu makocha wengi wa Kitanzania waliopo kwenye ushindani wanafanya vizuri kabisa,” anasema Josiah na kuongeza;

“Kwa nje nilikuwa shabiki wa Alex Ferguson napenda misimamo yake pamoja na Jose Mourinho, pia nawapenda Carlo Ancelotti, Pep Guardiola na Jurgen Klopp. Hawa wote ninajifunza kitu kutoka kwao kila mtu ana kitu chake cha kujifunza kwake,” anasema

CHAMPIONSHIP LIGI DUME

Kocha huyo anasema Ligi ya Championship ni moja ya michuano dume kwa sasa kutokana na ushindani na ugumu uliopo unaoletwa na hamasa ya kila mkoa kutaka kuwa na timu ya Ligi Kuu huku kukiwa na ushawishi wa wanasiasa na nguvu ya uchumi.

“Nawapongeza TFF (Shirikisho la Soka nchini) na Bodi ya Ligi kwa namna wanavyosimamia kulinganisha na kipindi cha nyuma maana kuna mabadiliko makubwa hakuna matukio ya ajabu na changamoto zimebaki kidogo,”

“Sasahivi kuna wadhamini, unapata ushahidi wa matukio, ligi inachezwa kwenye viwanja vizuri, timu zina wataalam na adhabu kali zinatolewa,” anasema kocha huyo

AISHAURI BIASHARA UNITED

“Ushauri ambao ninaweza kuwapa Biashara ni kutafuta vyanzo vya mapato vikubwa kwasababu Ligi ya Championship inahitaji fedha, wachezaji wazuri, benchi la ufundi bora. Wakiweza kuwabakisha wachezaji waliokuwepo na kupata benchi la ufundi zuri uongozi ukasimama imara inaweza kupambana kurudi Ligi Kuu,”

“Ni timu ambayo inapanedwa na mashabiki wa mkoa wa Mara, kwahiyo nashauri kwamba viongozi walioshikilia na wafanye kazi kwenye hayo maeneo hususan kiuchumi na kutafuta wachezaji watakaosaidia timu, wasifanye skauting ya ilimradi tu,” anasema Josiah

MISIMAMO YAKE

“Mimi ni mtu mwenye misimamo kuanzia kwa wachezaji wangu na benchi la ufundi nasisitiza nidhamu kazini kuanzia kuwahi mazoezini, mazingira ya kufanya kazi kila mmoja awajibike. Wachezaji ikishaisha pre season ikija muda wa kazi ni kuweka akili zao kwenye kazi ili tufanikiwe,”

“Timu ikinihitaji cha kwanza kabisa nazingatia mazingira ya kazi, nawaambia viongozi mimi ni mtu wa misimamo na nidhamu, nauliza ni nani anaweza kuniongoza na kunilinda kwenye misimamo yangu ili nifanikiwe,”

“Kwahiyo mimi huwa natafuta kwanza uhuru wa mamlaka ya kufanya kazi kabla ya kujua utanilipa kiasi gani. Nijue kwanza yale ninayokuja kufanya kwenye taasisi yako ni nani yuko tayari kunilinda kwenye uongozi ninapotimiza majukumu yangu ama uongozi nao utanigeuka,” anaeleza kocha huyo

UJUMBE KWA MAKOCHA WAZAWA

“Nafikiri makocha wazawa wanapaswa kuaminiwa lakini kabla ya hilo wanapaswa wajiamini kwa kile wanachokifanya lakini kama unapata kazi kwa ujanja ujanja maana yake kujiamini hakutokuwepo. Tunatakiwa tusimamie misimamo yetu, unaamini unafanya kazi simama na misimamo yako,”

“Kama sijaridhishwa na mazingira ya kazi siwezi kwenda kufanya hiyo kazi, sifanyi kazi kwa sababu nina shida na fedha, nikitanguliza njaa mbele nitakosa uhuru wa kutimiza majukumu yangu. Sisi wenyewe makocha tunataka kuaminiwa lakini tujiweke kwenye hali ya kujiamini sisi weyewe,”

“Viongozi siku zote wanakuwa na majaribu wanataka uingie kwenye njia zao wakupangie uingie kwenye udhaifu wao. Cha kwanza sisi wenyewe makocha tuwe na utaratibu wetu na tufanye kazi kwenye misingi yetu, njaa isitupeleke tupate kazi, bali tupate kazi kutokana na uwezo wetu,” anashauri Josiah

Related Posts