RT yaongeza nguvu kambi ya Taifa ya Olimpiki

Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limekabidhi vifaa vya michezo katika kambi ya timu ya Taifa ya riadha inayojiandaa kushiriki Michezo ya Olimpiki kama  sehemu ya kukiongezea nguvu kikosi hicho.

Kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wanne wa marathoni ya mbio ndefu za kilomita 42 na wamebeba jukumu la kwenda kuandika historia ya kuleta tena medali baada ya kupita zaidi ya miaka 40.

Mara ya mwisho medali hizo zililetwa na wanariadha Suleiman Nyambui aliyeliletea Taifa medali ya fedha mbio za mita 5000 na Filbert Bayi mita 3000 kwenye Olimpiki za Moscow urusi mwaka 1980.

Akizungumza wakati wa kugawa vifaa hivyo katika kambi ya timu hiyo iliyoko Sakina, jijini hapa, Mjumbe wa RT, Alfredo Shahanga amesema anaamini itawaongezea morali na watarudi na medali.

Amesema vifaa hivyo ni tisheti, fulana, traki suti, viatu na jaketi watakazovaa wakati wa mazoezi,  kambini na kwenye michezo hiyo.

“Sisi kama RT tunawaombea mafanikio wachezaji wetu ambao wamefikisha viwango vya kutuwakilisha Olimpiki,” amesema Shahanga.

Nahodha wa timu hiyo, Alphonce Simbu ameipongeza RT kwa kutambua umuhimu wao na kuamua kuongeza nguvu katika vifaa vya michezo ambavyo vitawasaidia kushinda na kurudi na medali.

“Siku za nyuma tulikuwa hatuna kampuni ambayo inabeba alama kwa ajili ya Tanzania lakini kwa sasa tunawashukuru RT kwa juhudi kubwa ambazo wamefanya na kupata kampuni ambayo imetuletea vifaa hivi,” amesema Simbu.

Kwa upande wake kocha wa timu hiyo, Antony Mwingereza amesema kutokana na vifaa hivyo morali itaongezeka kwa wachezaji na maandalizi yanaendelea vyema.

Bingwa wa marathoni nchini, Magdalena Shauri amesema maandalizi kwa upande wao kama wachezaji yanaendelea kama kawaida na anaamini kutokana na ubora wao wote basi lazima watarudi na medali.

Vifaa hivyo vya michezo kwa ajili ya timu ya Taifa inayokwenda Paris huku wakitazamiwa kukimbia Agosti 10 kwa upande wa wanaume na Agosti 11 kwa upande wa wanawake vimetolewa na mdhamini wa RT, kampuni ya X tep.

Related Posts