Tanzania yapata mtambo wa kisasa wa uchorongaji madini

Geita. Tanzania imepata mtambo mkubwa wa uchorongaji madini ya dhahabu wenye uwezo wa kujiendesha, huku ukitarajiwa kuwa mwarobaini wa ajali mgodini na kuongeza uzalishaji wa dhahabu.

Mtambo huo, wenye uwezo wa kuchoronga mita 400 kwenda chini, umenunuliwa na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) kwa gharama ya Sh4 bilioni na utatumika kuchoronga madini katika mgodi wa dhahabu wa Geita (GGML).

Akizungumza leo Julai 23,2024 wakati wa uzinduzi wa mtambo huo wa kisasa, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Venance Mwase amesema mbali na kujiendesha kwa  kutumia ‘rimoti’ una uwezo pia wa kuendeshwa  na mtu kwa njia ya kawaida.

“Mtambo huu una teknolojia ya juu ambapo sampuli hazishikwi kwa mkono, bali zinachakatwa moja kwa moja na kupelekwa sehemu nyingine kwa uchambuzi. Hii inaashiria mageuzi makubwa ya kiteknolojia ambayo yataendelea kwa zaidi ya miaka 50 na kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Dk Mwase amesema mbali na mtambo huo, ipo mingine 14 inaletwa na lengo ni kuleta mageuzi kwenye sekta ya uchimbaji na kuhakikisha wachimbaji wanakuza uchumi wa nchi.

Amesema shirika hilo tangu lianze kufanya mageuzi, limefanikiwa kutoka kwenye utegemezi, miaka mitatu iliyopita walikuwa wakikusanya Sh1.6 bilioni kutoka kwenye vyanzo vya ndani na sasa wana uwezo wa kukusanya Sh61 bilioni kwa bajeti ya mwaka 2022/23.

Kutokana na mabadiliko hayo, kwa sasa wameweza kukusanya Sh90 bilioni na kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 wamelenga kukusanya Sh161 bilioni.

Shirika hilo limeanza kuwalipa wafanyakazi wake mishahara na marupurupi mengine kutoka kwenye mapato yake ya ndani.

“Tulipoanza mageuzi, wateja wetu ambao ni GGML walitupa kandarasi ya kwanza mwaka 2020 tukiwa na mtambo wa majaribio. Lakini sisi kama Stamico tumekaa na watumishi na kukubali kubadilika kwenda nchi ya asali na haturudi nyuma,” amesema Dk Mwase.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema uwepo wa mtambo huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika mageuzi na mapinduzi kwa sekta ya madini nchini.

Gombati amewataka watumishi kuutunza mtambo huo na kuutumia kwa matumizi sahihi na kuhakikisha unafanyiwa ukarabati, kwa kuzingatia miongozo ili uweze kudumu kwa muda mrefu.

Hata hivyo, amelitaka shirika hilo kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuwekeza kwenye mafunzo ya muda mrefu na mfupi kulingana na mabadiliko ya teknolojia zinazotokea katika uendeshaji wa mitambo.

Pia, amewataka kukuza biashara kwa kuzingatia misingi ya kufikia malengo ya wateja ili kuingia kwenye soko la ushindani.

Mratibu wa Jiolojia kutoka Mgodi wa GGML, Erick Kalondwa amesema uamuzi wa Stamico wa kuleta mtambo mpya wenye nguvu, utajibu na kumaliza changamoto ya uchorongaji katika mgodi huo.

“Mtambo huu utaleta thamani kwa GGML, lakini pia kwa Stamico na Serikali ya Tanzania. Nina imani tutapata mita zaidi na itapunguza gharama. Tunahitaji uchorongaji wa haraka lakini unaozingatia usalama kwanza na kifaa hiki ndiyo suluhisho,” amesema Kalondwa.

Related Posts