HAGILA AITABIRIA MAKUBWA PAMBA JIJI

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

MJUMBE wa Bodi ya Pamba Jiji FC,Evarist Hagila amesema Tamasha la Pamba Day ni chachu ya kuwafanya mashabiki kutambua timu yao imerejea ligi kuu.

Pia wamesajili wachezaji wa viwango,usajili uliosimamiwa kwa weledi na wataalamu wa soka chini ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Goran Kopunovic,raia wa Serbia.

Hagila ametoa kauli hiyo leo baada ya uzinduzi wa uuzwaji wa tiketi za kuingilia katika tamasha la Pamba Day, litakalotumika kuwatambulisha wachezaji wa kikosi hicho.

Amesema tamasha la Pamba litakuwa chachu kwa mashabiki kuwafanya watambue timu yao imerejea ligi kuu baada ya kuikosa kwa miaka zaidi ya 22,hivyo litumika kuwatambulisha wachezaji wa kikosi hicho.

Hagila amesema baada ya Pamba Jiji Fc kufuzu kucheza ligi kuu anaamini kwa usajili walioufanya itaonesha maajabu kutokana na aina na viwango vya wachezaji mseto wa damu change na wakongwe wachache

“Tumefanya usajili mzuri uliosimamiwa na kocha na wataalamu wenye weledi,hatuwezi kuwa wachawi wala waganga wapiga lamli,tutaonesha tulichofaya katika usajili naamini tuna timu nzuri.

“Pia mpira ni hamasa,hicho ndicho anachokitafuta Mkuu wa Mkoa (Said Mtanda) hapa,siku ya Pamba Day hapo Agosti 10,mwaka huu, tutakwenda kuujaza Uwanja wa CCM Kirumba,” amesema Hagila.

Mjumbe huyo wa Bodi ya Pamba Jiji amesema uzoefu walionao wa kucheza ligi ya Championship kwa miaka mitatu ni somo tosha kwao na hivyo ligi kuu lazima mpira uchezwe kwa vitendo si maneno.

Aidha amenunua tiketi za wadau na mashabiki walioambatana na kuiunga mkono Pamba Jiji katika vita ya kupanda daraja zilizomgharimu shilingi milioni Moja ziwawezeshe kushu kuingia uwanjani kushuhudia tamasha la Pamba Day hapo Agosti 10, mwaka huu.

“Tiketi hizo nimenunua za wapambanaji wa Pamba Jiji waliojitoa kuipambania timu katika michezo mbalimbali tukiwa bega kwa bega hatimaye kupanda ligi kuu,”amesema. Naye mchezaji wa zamani wa Pamba almaarufu Tour Poissant Lindanda (TP Lindanda),Abuu Seif Mazige amewaushauri viongozi wa Pamba Jiji kuwakumbuka kwa kuwafanyia dua wachezaji takribani 40 waliotumikia timu hiyo ambao wametangulia mbele ya haki ili ifanye vizuri.

 

Related Posts