Dar es Salaam. Baada ya majaribio ya chanjo ya sindano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) ‘PrEPVacc’ yaliyofanyika kwa miaka minne Mashariki na Kusini mwa Afrika, imebainika haijafanikiwa kupunguza maambukizi ya virusi hivyo miongoni mwa waliofanyiwa utafiti.
Majaribio ya chanjo hiyo yalisitishwa Novemba, 2023 na baadaye kutangazwa hadharani Desemba mwaka huo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu zilizoshiriki majaribio hayo kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 katika mikoa ya Mbeya na Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kiongozi wa mawasiliano wa mradi wa majaribio ya chanjo hiyo, Tom Miller, inaeleza maeneo mengine yaliyoshiriki majaribio hayo ni Masaka, nchini Uganda na Durban, Afrika Kusini.
Utafiti wa PrEPVacc, uliongozwa na watafiti kutoka Afrika kwa msaada wa wenzao wa Ulaya ukihusisha majaribio matatu.
Matokeo ya majaribio hayo yametangazwa leo Julai 23, 2024 katika mkutano kuhusu masuala ya Ukimwi uliofanyika Munich, Ujerumani.
Imeelezwa hakuna kati ya aina mbili za majaribio ya chanjo hiyo iliyofanikiwa kupunguza maambukizi ya VVU.
Mkuu wa mradi huo nchini, Dk Lucas Maganga kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr-Mbeya) hakupatikana kuzungumzia majaribio ya chanjo hiyo.
Kwa zaidi ya miaka mitano Tanzania imekuwa ikitumia dawa kinga aina ya PrEP, iliyo katika mfumo wa vidonge.
Mradi wa majaribio ya PrEPVacc ulishirikisha watu 1,512 wenye afya njema wa umri wa miaka 18 hadi 40, ambao wanajihusisha na tabia hatarishi zinazoweza kusababisha maambukizi ya VVU.
Idadi ya washiriki ilijumuisha asilimia 87 ya wanawake na asilimia 13 wanaume.
Kwa Tanzania walioshiriki ni wanawake pekee, huku maeneo mengine yalijumuisha wanaume na wanawake.
Mtafiti Mkuu wa mradi wa majaribio ya chanjo ya PrEPVacc, Profesa Pontiano Kaleebu amesema maswali ya chanjo yaliyoulizwa katika majaribio yamejibiwa na kilicho wazi ni kwamba haitaendelezwa.
“Matokeo yamekuwa ya kushangaza na yamekuwa ya kukatisha tamaa. Lakini hiyo ni sayansi. Umekuwa utafiti mzuri, unaofuata viwango vya juu vya kimataifa.”
“Lazima tusonge mbele kwa sababu dunia inahitaji kuwa na chaguo katika kisanduku chake cha zana za kuzuia maambukizi ya VVU. Chanjo dhidi ya VVU inasalia kuwa sehemu inayotafutwa na muhimu katika kisanduku hicho cha zana,” amesema Profesa Kaleebu.
Mkurugenzi wa mradi huo wa majaribio ya PrEPVacc, Dk Eugene Ruzagira akiwasilisha matokeo ya chanjo hiyo kwenye mkutano wa Ukimwi 2024, amesema ilisitishwa Novemba, 2023 baada ya kuonekana haizuii maambukizi.
Kiongozi wa mradi huo aliye katika kitengo cha majaribio ya kimatibabu cha Baraza la Utafiti wa Kitiba katika Chuo Kikuu cha London, Profesa Sheena McCormack amesema:
“Hatuwezi kuondoa uwezekano wa matokeo, hivyo ni wazi tunahitaji kuendelea kuwaunga mkono washiriki na kupima VVU ili kufuatilia mwenendo.”
“Jumla ya idadi ya maambukizi katika majaribio ilikuwa ndogo zaidi kuliko tulivyotarajia, ambayo ni habari njema na ninatumaini hii inaonyesha kile kinachotokea katika jamii pana,” amesema.