SIO ZENGWE: Magoma amechelewa kuamka, lakini amefikirisha

MIAKA ya mwanzoni wa 1990 hadi mwisho haikuwa ajabu kusikia klabu ina kesi hata zaidi ya tano kwenye mahakama tofauti na hukumu zake kuibuka kwa nyakati tofauti na wakati mwingine kuvuruga kabisa mipango ya klabu.

Ukiacha mgogoro uliosababisha Yanga igawanyike na kikosi kizima cha kwanza kuondoka, ule wa miaka ya 1990 mwanzoni ulikuwa mkubwa zaidi kwa zama za kizazi hiki. Mgogoro huo ulitokana na wafadhili watano wa Yanga kujiondoa kwa lengo la kushinikiza wanachama wauondoe uongozi wa Jabir Katundu na George Mpondela. Kweli kuna wanachama walishawishika na kuanza kuweka shinikizo viongozi hao waondoke.

Hata hivyo, Mpondela alisimama imara kupinga hujuma hizo na kuhubiri hoja za kutaka klabu ijitegemee iondokane na kutegemea wafadhili kwa kuwa ina mali nyingi za kuiwezesha kuzalisha fedha. Na hapo ndipo lilipoanza wazo la kuibadili katiba ili kuingiza muundo wa kampuni. Wazo lake likaungwa mkono na kundi moja la wanachama huku jingine, lililokuwa linanufaika kimaisha na uwepo wa wafadhili likapinga likisema linataka Yanga iendelee na muundo wake wa asili na hivyo kundi hilo kuitwa Yanga Asili na jingine Yanga Kampuni.

Kulifuatia visa vingi, kikiwemo cha timu kutekwa na kwenda kufichwa hoteli moja jijini Dar es salaam ambayo si viongozi wala waandishi hawakuijua. Timu ilikuja kuibuka Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) siku ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Sigara, lakini ikachapwa mabao 3-0.

Vituko vingine vya kuzuia mikutano ya wanachama vikaanza huku kesi za kupinga marekebisho ya katiba zikimiminika mahakamani. Juma Magoma, Salum Ngereza, Frank Chacha na Geofrey Mwaipopo ni baadhi ya wanachama waliohusika katika kufungua kesi zilizovuruga mikutano mikuu au uchaguzi wa viongozi.

Katika kesi zote, egemeo lao kuu limekuwa ni katiba ya mwaka 1968. Kila wanapotaka kupinga jambo la mabadiliko kwenye muundo wa Yanga au jambo jingine lolote hutumia katiba ya mwaka 1968 kubatilisha uhalali wa viongozi waliopo madarakani kwamba hawakuchaguliwa kwa katiba hiyo na hivyo kutokuwa na nguvu ya kuitisha ama mkutano mkuu au uchaguzi. Na kesi zao huwa dhidi ya baraza la wadhamini.

Hivyo, chochote kinachofanyika sasa kinaweza kuja kubatilishwa baadaye kwa kuwa mabadiliko yote yaliyofanyika kuanzia miaka ya mwanzo wa milenia hii mpya ama yamefanywa na viongozi batili kwa kuwa walichaguliwa bila ya kutumia katiba ya mwaka 1968 ama ni batili kwa kuwa katiba yenyewe haitambuliki.

Huko nyuma, Magoma na wenzake walifanikiwa kuvuruga mikutano au chaguzi na wakafanikiwa kugawa wanachama ambao kwa sababu moja au nyingine walikuwa wakitofautiana na viongozi wa wakati huo. Lakini hali inaelekea kubadilika.

Wanachama wanaonekana kuchoshwa na migogoro ya uongozi na wanachotaka ni kuona klabu ikisonga mbele na kuwafurahisha uwanjani, hasa katika kipindi hiki ambacho Yanga imeonekana kuwa na mafanikio makubwa.

Zaidi ya hoja kwamba katiba ya sasa haijasajiliwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita) kama ilivyosajiliwa katiba ya mwaka 1968, hakuna hoja nzito waliyonayo Magoma na Mwaipopo inayoweza kushawishi wanachama wawaunge mkono labda wale wachache wenye chuki binafsi na viongozi wa sasa.

Hoja kwamba katiba inawabagua wanachama kwa kuwa mkutano mkuu sasa unahusisha viongozi watano wa matawi, haina nguvu kubwa kwa kuwa idadi ya wanachama ishakuwa kubwa na haiwezekani wote waitwe mkutanoni kufanya maamuzi. Labda kama Magoma na mwenzake wangeshauri mikutano mikuu na ile ya uchaguzi ihusishe baadhi ya wanachama kielektroniki kama ambavyo Real Madrid hupiga kura kumchagua rais wao.

Hoja kwamba Yanga inaongozwa na wanachama waliojimega Simba, haina nguvu yoyote kwamba lengo la klabu ni kupata wanachama na mashabiki wengi kadiri iwezekanavyo, na kumchomoa mwanachama kutoka timu pinzani ni mafanikio makubwa.

Hoja kwamba viongozi ni vijana au watoto wadogo, huo ni ubaguzi mkubwa zaidi kuliko ule wa mkutano mkuu kutoshirikisha wanachama wote.

Anadai kuwa wanachama wanashindwa kuhoji masuala ya kifedha, hasa udhamini wa jezi ambao anadai Wanayanga hawajui mdhamini huingiza kontena ngapi na idadi gani ya jezi ili wajue fedha kamili anazopata dhidi ya kiwango kinachoenda Yanga. Hapo anataka kumaanisha idara ya uhasibu haijui lolote wala hakuna kiongozi anayehoji, au hataukaguzi haufanyiki kwa njia ambayo inatoa majibu ya maswali yake.

Kwa kifupi, Yanga haiwezi kuendelea kuwa ileile ya mwaka 1968 ambao yeye Magoma na wenzake walikuwa wadogo. Ni lazima ibadilike. Huu ni usingizi mzito ambao Magoma bado hajazinduka na anadhani ataendelea kuufaidi kwa nyaraka hiyo.

Mambo yamebadilika sana na ndio maana kila taasisi iko kwenye harakati za kubadilisha muundo wake wa uongozi na hata umiliki ili uendane na dunia ya leo ya sayansi na teknolojia. Na Magoma anaonekana hataki kuamka na kuungana na wengine kulisukuma mbele gurudumu la Yanga, huku akiegemea usajili ambao unaweza kutekelezwa mara moja na hivyo nguvu zake za kuvuruga klabu zikawa zimefikia mwisho.

Ni muhimu kwa Magoma kwenda na wakati na mwitikio mdogo wa Wanayanga katika hukumu ya kesi inayobatilisha wadhamini na viongozi, ni ishara tosha kwamba wengi wamebadilika na hivyo hana budi kuungana nao.

Lakini pia Magoma ametoa angalizo kwamba tunapofanya mabadiliko au maamuzi makubwa tusitangulize ushabiki na kutumia nguvu za ziada za nje kupitisha kile tunachokusudia kwa kuwa kwa kufanya hivyo tunajikuta tukikumbatia kasoro ambazo zinaweza kuja kubatilisha kila kitu baadaye.

Mikutano mikuu ya klabu hutawaliwa na kelele za kuzomea wale wenye mawazo tofauti, badala ya kuyasikiliza kwa makini. Enzi za rais wa zamani wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Joseph Blatter zilikuwa za aina yake kwenye mikutano mikuu iliyolenga kufanya maamuzi mazito.

Licha ya kwamba uongozi wake ulifanyia utafiti wa kina kila jambo ambalo ulitaka lifanyiwe uamuzi na mkutano mkuu, bado Blatter aliweka kipaumbele kwa wajumbe ambao walikuwa na hoja zinazolipinga suala hilo. Hivyo wajumbe waliokuwa na hoja tofauti na uongozi ndio waliokuwa wakipewa nafasi kwanza ya kutoa hoja zao na baadaye ndipo wanaounga mkono hoja walipewa nafasi za kuzijibu na mwishoni yeye mwenyewe kuhitimisha.

Huu ndio ustaarabu ambao viongozi wetu wa klabu yafaa wauchukue. Lazima kuwasilikiza kwanza wenye mawazo tofauti na yajadiliwe kwa makini ili asiachwe mtu nyuma akaenda zake mahakamani.

Related Posts