Masauni aonya wanafunzi matumizi ya dawa za kulevya

Unguja. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amewaonya wanafunzi waliopo shuleni, vyuoni na taasisi nyingine za elimu kuacha kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, ambazo husababisha nguvu kazi ya Taifa kupotea.

Pia, ameitaka jamii kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika vita dhidi ya dawa za kulevya zinazoathiri maendeleo ya uchumi wa nchi.

Ametoa kauli hiyo Zanzibar jana Jumatatu Julai 22, 2024 kwenye mkutano wa hadhara.

Masauni  amesema vijana wamethiriwa na dawa za kulevya kwa kuvuta kupitia puani, mdomoni na kujidunga sindano.

“Vijana hususani walipo shuleni na vyuoni ni tegemeo la kuwa viongozi wa baadaye wa Taifa hili, lakini hawawezi kuwa kwenye nafasi hizo wakijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya,” amesema.

Masauni amesema ni muhimu jamii kushikamana kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.

Amesema utafiti unaonyesha janga la matumizi ya dawa za kulevya limehamia kwa wanafunzi ambao wengine wana shahada za taaluma mbalimbali lakini wamejiingiza katika uraibu. Hata hivyo, hakueleza ni tafiti gani na zilifanyika lini.

Amesema jambo hilo linahatarisha uhai wa Taifa.

“Serikali imeunganisha nguvu ya pamoja kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya, wito wangu kwa wazazi na wanajamii kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kudhibiti janga hilo,” amesema.

Khadija Salum Vuai, mwananchi aliyeshiriki mkutano huo amesema vijana wanaathirika na dawa hizo kwa sababu ya makundi wanayokutana nayo wanapokwenda shuleni.

“Wanakutana wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali, huko kila mmoja anakuwa na tabia na malezi yake, lakini makundi haya ndiyo yanaponza wengi na kujikuta wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa hizo,” amesema.

Abdulla Mussa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) amesema tabia za kuiga ndizo zinawaponza wanafunzi wengi kwa kuwa wanashindwa kuwa na misimamo.

Waziri Masauni pia amezungumzia matendo ya udhalilishaji, yakiwamo ulawiti, ubakaji na mapenzi ya jinsia moja ambayo amesema yanakithiri, huku jamii na familia zikiwaficha wanaojihusisha na vitendo hivyo.

“Kuna mmomonyoko wa maadili unaosababisha matukio yaendelee kutokea, na kumekuwa na desturi kwa baadhi ya watu wanaofanya matendo ya ubakaji na ulawiti, hususani kwa watoto tunawakumbatia na kuwaficha,” amesema.

Related Posts