ACT-Wazalendo yakemea siasa utekelezaji miradi

Unguja. Chama cha ACT-Wazalendo kimesema masuala ya kisiasa yanachangia kukwama miradi mikubwa ya maendeleo na kusababisha miradi ya mabilioni ya fedha za wananchi kukwama.

Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Julai 21, 2024 kwenye Uwanja wa Mwenge, Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.

Akiwahutubia wafuasi, wanachama na wananchi waliohudhuria mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Zanzibar, Ismail Jussa ametaja kukwama ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Pemba akidai ni kutokana na uingiliaji wa kisiasa wa mikataba kati ya kampuni zinazoshughulikia mradi huo.

Juni 2023, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliingia mkataba wa Dola milioni 428 za Marekani (Sh1.01 trilioni) na UK Export Financing kupanua Uwanja wa Ndege wa Pemba na kujenga mitandao mbalimbali ya barabara Unguja na Pemba.

Hata hivyo, ujenzi huo bado haujaanza kutokana na sababu za migogoro ya kampuni hizo.

Ufadhili wa miradi hii unawezeshwa na Citibank London na Deutsche Bank London, iliyodhaminiwa na Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Fedha la Uingereza la Mauzo ya Nje (UKEF).

Januari 10, 2024 Mahakama Kuu ya Zanzibar ilitoa amri za muda kusimamisha maendeleo ya mradi kusubiri utatuzi wa mgogoro wa kisheria kati ya kampuni hizo mbili.

Malalamiko yaliyotajwa ni pamoja na madai ya matumizi mabaya ya nyadhifa za wanahisa wengi, kuingiliwa kisiasa na kushindwa kuzingatia masharti ya kimkataba.

Licha ya majaribio ya kusuluhisha migogoro nje ya Mahakama bado migogoro hiyo iliendelea.

Mikataba ya kibiashara na makandarasi Mecco na Propav, inayofanya kazi kwa ubia, iliidhinishwa na kusainiwa na Serikali ya Zanzibar Septemba 2022 na Januari 2023.

Miradi hiyo ni pamoja na Barabara ya Tunguu-Makunduchi yenye urefu wa kilomita 48 katika Mkoa wa Kusini Unguja, Barabara ya Kisauni-Fumba yenye urefu wa kilomita 12 katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Barabara ya Mkoani-Chake Chake, Pemba yenye urefu wa kilomita 43.5.

“Hizi ni fedha za mkopo lakini italazimika kulipwa, kwa hiyo masuala haya hatupaswi kuyafumbia macho yanaumiza Taifa hili. Na watu wanaohusika na mambo haya ACT tutakapoingia madarakani watawajibika kwa hili,” amesema Jussa.

Alipotafutwa Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hilary alielekeza atafutwe Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Muhamed Khalid Salum.

Alipotafutwa waziri huyo simu yake haikupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi haukujibiwa.

Hata hivyo, wakati akijibu hoja mbalimbali za wawakilishi zilizoibuka wakati wa Baraza la Wawakilishi lililojadili bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 kuhusu mradi huo, Dk Khalid alisema katika Uwanja wa Ndege wa Pemba kuna mambo yalikuwa yakiwekwa sawa kati ya kampuni za utekelezaji wa mradi huo bila kutaja mambo hayo.

Alisema utekelezaji wa mradi huo bado upo ndani ya mkataba, hivyo utaanza kutekelezwa Julai mwaka huu.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo -Taifa, Othman Masoud amesema ni haki ya wananchi kuamua kiongozi wanayemtaka na kwamba kufanya hivyo, ndiyo ufalme wa wananchi katika kutekeleza maamuzi yao ya ushiriki wa demokrasia ya kweli kwenye uchaguzi.

Amesema Wazanzibari wakiwamo watu wa Kusini wameendelea kuamka na kwamba ni muhimu kushirikiana katika kuiunga mkono zaidi ACT-Wazalendo ili iweze kushinda kwenye uchaguzi mwakani na kuleta mabadiliko katika uongozi na kuchangia kasi ya kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.

“Chama kimejipambanua kuendeleza kutimiza wajibu wake wa kuwasemea wananchi na kuleta mawazo mbadala kwa kuwa ndiyo kazi za vyama vya siasa,” amesema.

Amesema suala la kuendeleza ghiliba na ujanja ikiwamo masuala ya kura za mapema na kuwanyima wananchi haki ya vitambulisho ambavyo ndiyo msingi wa kuwa mpigakura ni mambo ambayo ACT-Wazalendo hakiyakubali kuendelea kuwapo Zanzibar.

Amewataka wananchi hasa wa Mkoa wa Kusini kuelimishana na kuhakikisha watu hawaendelei kutumika kurejesha nyuma juhudi za kuleta mabadiliko ya kidemokrasia.

Related Posts