Unguja. Wizara ya Maji, Nishati na Madini imetia saini mikataba ya ujenzi wa miundombinu ya nishati na Kampuni ya Umeme, Zhonglian Technology (ZTT) na Sieyuan kutoka China ili kuondoa tatizo la umeme.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba hiyo Julai 21, 2024, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara, amesema utekelezaji wa mradi huo utafungua njia za kiuchumi na kusaidia kuinua uchumi wa nchi hasa katika sekta ya utalii.
“Uchumi wa nchi ili uweze kukua na kuwa endelevu lazima kuwepo na upatikanaji wa miundombinu ya umeme iliyobora,” amesema Waziri Kaduara.
Ametumia fursa hiyo kuwataka makandarasi kutekeleza mradi huo kwa wakati ili kutatua changamoto za umeme mdogo kwa wananchi wa Zanzibar.
Pia, amewataka wafanyakazi wa shirika la umeme kutoa ushirikiano kufanikisha mradi huo kwa wakati uliopangwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi amesema lengo la mradi huo ni kutatua changamoto za umeme mdogo kwa baadhi ya maeneo na upotevu wa nishati hiyo.
Katika utekelezwaji wa mradi huo, laini ya umeme wa kilovoti 152 itajengwa kwa urefu wa kilomita 99.9 na vituo vya kupozea umeme ambavyo vitakuwepo katika maeneo ya Makunduchi na Matemwe.
“Katika hili tunakwenda kufungua njia za utalii kwa Mkoa wa Kaskazini na Kusini, kupunguza upotevu wa umeme na kuweka nguzo za umeme kwa wanaohitaji,” amesema Kilangi.
Amewataka wananchi ambao wameshalipwa fidia kuondoka katika maeneo hayo na ambao hawajapatiwa fidia utaratibu unaendelea hivi karibuni watapatiwa ili kupisha ujenzi wa mradi huo.
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar, Haji Juma Haji amesema kusainiwa kwa mikataba hiyo kutaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya umeme kwa kuwa utavutia wawekezaji wa viwanda vya kati na kusaidia katika kuongeza ajira nchini.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo kutawahamasisha wananchi kutumia nishati ya umeme katika shughuli mbalimbali zikiwamo za kupikia na kuokoa mazingira.
Amesema shirika limejipanga kukamilisha mradi huo kwa wakati na kuleta tija kwa watumiaji jambo ambalo litaleta mafanikio kama yalivyokusudiwa na Serikali.
Mikataba hiyo miwili itatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja.