Mbeya. Wakati Serikali ikiendelea kuratibu makazi ya waathiriwa wa maporomoko ya tope linalotoka Mlima Kawetere jijini hapa, waathiriwa hao wameondoka kwenye kambi ya muda katika Shule ya Msingi Tambukareli walikokuwa wamewekwa.
Maporomoko hayo yaliyotokea alfajiri ya Aprili 14 mwaka huu katika Kata ya Itezi jijini Mbeya na kusababisha nyumba zaidi ya 20 na Shule ya Msingi Generation kufunikwa na tope.
Mbali na nyumba hizo, pia mali za ndani na mifugo zilisombwa na kufanya wananchi zaidi ya 50 kukosa makazi.
Mmoja wa waathirika, Hamis Gumbo amesema baada ya huduma walizopata kutoka kwa wadau kwa sasa wanasubiri hatima ya kujua watawekwa wapi na kwamba wako tayari kupelekwa popote.
“Sisi tunawashukuru wote walioguswa na changamoto yetu, Serikali pia ilitusaidia sana na tunasubiri huruma yao kuona watatupa maeneo gani ili tuanze upya maisha.
“Tunahitaji misaada kwa sababu watu tulipoteza kila kitu, hatuna pa kuanzia hivyo kama Serikali watatupa viwanja tukapata na kianzio itatusaidia sana,” amesema Gumbo.
Mratibu wa maafa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mboka Mwakajila ameliambia Mwananchi leo Aprili 25, 2024 amesema tayari waathirika hao wameondoka katika kambi hiyo Jumapili Aprili 21, 2024 baada ya kukabidhiwa misaada inayoweza kuwatosha kwa siku 90.
“Tayari wameondoka na shuleni ratiba zinazoendelea ni masomo tu, kuna ambao wameenda kwa ndugu zao na wengine wamepanga nyumba, japokuwa tunaendelea kupokea watu binafsi na vikundi vinavyoleta misaada.
“Tulitoa magodoro, mablanketi na vyakula vya kujitosheleza kwa takribani miezi mitatu na hii (misaada) inayokuja tutawaita tena kuwakabidhi,” amesema Mwakajila.
Kuhusu suala la kuwapatia maeneo, Mwakajala amesema mpango uko chini ya Idara ya Mipango Miji ya jiji la Mbeya.
“Hilo nadhani liko katika mchakato kwa wahusika idara ya Ardhi Mipango Miji, kwa sababu lazima wafanye utafiti kujua maeneo yaliyo salama ili wawaweke huko,” amesema alipoulizwa na Mwananchi.
Mkuu wa idara hiyo, Dickley Nyato amesema wanaendelea kushughulikia suala hilo lakini anayefahamu hatua lilipofikia ni mkurugenzi wa jiji ambaye hata hivyo hajapatikana kupitia simu yake kulizungumzia.
Wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliwatangazia wakazi hao kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameuongozi wa Mkoa wa Mbeya kutoa viwanja kwa waathirika wa tope hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera alimesema maelekezo wameyapokea watahakikisha wanayatekeleza ndani ya wiki tatu ili wananchi wote 21 waliopoteza nyumba zao wapataiwe viwanja maeneo mengine.