Dar es Salaam. Siku 1,220 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani zimekuwa za panga, pangua kwenye baraza lake la mawaziri kutafuta ufanisi huku mabadiliko hayo yakidaiwa kuwanyima wateule hao nafasi ya kutosha kuonyesha ubunifu na kuacha sifa katika taasisi wanazoziongoza.
Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 na hadi Julai 21, 2024 alikuwa amefikisha siku 1,220 akiwa ameteua, kutengua, kuwahamisha wizara mawaziri, naibu mawaziri na amewapandisha baadhi yao kutoka naibu na kuwa mawaziri kamili.
Unaweza kusema hakuna ambaye aliyepo barazani hajaguswa. Baraza alilolipokea kutoka kwa mtangulizi wake, kwa sehemu kubwa wamekwishahamishwa, amewaweka kando na amefanya mabadiliko katika maeneo mbalimbali.
Waziri aliyesalia kwenye wizara yake ni Dk Mwigulu Nchemba wa Fedha, ambaye hata hivyo, alipunguziwa kipengele cha Mipango na kupewa Profesa Kitila Mkumbo. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yeye amesalia kinara wa bara hilo.
Mabadiliko hayo ya mara kwa mara yamejaliwa kwa namna tofauti na wachambuzi ukiibua hoja za wanaodhano hakuna tatizo na wanaoeleza kasoro zake.
Mjadala huio umeibuka baada ya mabadiliko yaliyofanywa Jumapili Julai 21, 2024 kwa kuwaweka kando mawaziri wawili, Januari Makamba (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki) na Nape Nnauye wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wengine kadhaa, ikiwa ni siku 20 tangu Rais Samia alipofanya mabadiliko mengine kwenye baraza hilo.
Akizungumza mabadiliko ya kila mara, aliywahi kuwa katibu mkuu wa Utumishi, Ruth Mollel amesema hatua hiyo inaweza kupunguza ufanisi katika utumishi wa umma.
“Rais ndio mwajiri namba moja, anayo mamlaka ya kubadilisha Baraza na watumishi wa umma kwa jinsi anavyoona inafaa, lakini hamisha hamisha ya mara kwa mara inaweza kusababisha kutokuwa makini kwa maofisa wenyewe.
“Mtu atakaa kwenye kiti hajui kama atakaa au hatakaa, kwa hiyo anaweza kuwa na hofu ya kufanya uamuzi mkubwa mahali alipo. Vilevile anaweza asiielewe wizara vizuri,” amesema Mollel.
Akijenga hoja amesema: “Ili uweze kuielewa wizara vizuri kazi zake zote na mifumo yake yote, kwa mtu aliye na uelewa wa haraka anagalau uwe na miezi sita au mwaka mmoja.
Hata hivyo, amesema katika utumishi kuna watendaji na kuna wanasiasa kama mawaziri wanaokaa miaka mitano kulingana na matakwa na Rais anayewateua.
“Kama watendaji ni wazuri hata kama huku juu mawaziri wanabadilishwa, kazi zitaenda vizuri tu, kwa sababu utendaji mkubwa unafanywa na watumishi wa umma.
Kwa hiyo tuwe na utumishi wa umma wanaowatumikia wananchi, kwa sababu wale wanafanya kazi za siku kwa siku za Serikali, iwe kuna CCM au Chadema au ACT Wazalendo, kazi zinaendelea kama kawaida,” amesema.
Mollel aliyewahi pia kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chadema, ameeleza haja ya kuwa na mfumo mzuri wa upekuzi wa watumishi kabla ya kuwateua ili kuepuka kuwaondoa mara kwa mara.
“Mfumo wa uteuzi nao unapaswa kuwa imara ili kuhakikisha kuwa tunateua mtu sahihi katika nafasi husika,” amsema.
Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga anaona hakuna shida kwa mabadiliko ya mara kwa mara, cha msingi ni kuangalia uwezo wa watu.
“Haina matatizo kabisa kwa sababu Serikali inafanya kazi kwa maandishi na wizara inakuwa na mikakati na mipango kazi ambayo iko pale na yeyote anayekuja anaisimamia tu.”
“Watendaji ni walewale, katibu mkuu, wakurugezi, makamishna, mawaziri wanakuja hapo ni usimamizi wa kufanya kazi kwa kuweka ufuatiliaji. Waziri yoyote mwenyewe akili timamu, ukimtoa hapo na kumpeleka kwingine hawezi kushindwa kufanya kazi, kwa sababu unavikuta vyote viko hapo, ni kuongezea tu vichache,” anasema.
Mbunge huyo wa zamani wa Misungwi (CCM), anasema: “Tatizo labda ni uwezo wa watu wetu, lakini mfano mimi unanitoa hapo kila wiki na kunipeleke kwingine, sina tatizo, kwa sababu kuna mpango kazi wa Serikali na wote mnaujadili kwenye baraza la mawaziri na yote unajua.”
Anasema ukiwa kwenye Baraza la Mawaziri, unapoletwa mpango wa wizara fulani, hata kama sio waziri wa wizara hiyo, unaruhusiwa kuchangia na hiyo inakupa fursa kujua kinachofanyika kwa waziri mwenzako na ikitokea ukapelekwa huko kunakuwa hakuna tatizo.
Kitwanga anatolea mfano: “Uko shule unafundisha darasa la sita, ukitolewa na kuambiwa unakwenda kufundisha darasa la tano utashindwa? Huwezi shindwa, utamuuliza tu huyo mwalimu aliishia wapi na wewe unaendelea.
“Kikubwa tuzungumzie uwezo wa watu wetu ila kuhamishwa kutoka hapa kwenda kwingine hakuna shida. Wanaolalamiika ni mtazamo wao, kuna ile hali unakuwa mahala umepazoea, lakini mazoea wakati mwingine yanaleta shida,” anasema.
Kitwanga anajitolea mfano wake mwenyewe kuwa alianza kama naibu waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, akahamishiwa kuwa maibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira kisha akapelekwa Nishati na Madini akisimamia Nishati na baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani.
“Kuhamishwa huko hakukunipa tatizo lolote, na mimi ndiye nileleta gesi kutoa Mtwara hadi Dar es Salaam na ndio nilifungua mtambo namba I wa Kinyerezi. Baadaye nikahamishwa kusimamia madini, sikuwa naona tofauti,” anasema.
Akijadili suala hilo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema kuna faida na hasara ya mabadiliko ya mara kwa mara.
“Kwa upande wa pili, kunaweza kukawa na faida kwenye hiyo hamisha hamisha, kwa sababu mamlaka ya uteuzi inao uwezo wa kuteua na kutengua, kwa hiyo ni muhimu ikatumia hiyo fimbo kwa ajili ya kuleta nidhamu katika utumishi. Kwa mfano unaweza ukateua mtu, lakini unaona haendi katika mwelekeo unaotakiwa, inabidi tu amwondoe,” amesema.