Ubaya Ubwela: Mashabiki Simba waitika safari ya Mikumi

MASHABIKI wa Simba SC wameonekana kuitika kwa wingi huku wakivalia jezi za chama hilo katika safari ya kwenda Hifadhi ya Mikumi mkoani Morogoro kwa ajili ya uzinduzi wa Simba Day ambapo kilele kitakuwa Agosti 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika kutambua umuhimu wa kutangaza vivutio vya utalii nchini, Simba iliamua kufanya uchaguzi wa kuzindua wiki ya kuelekea tukio hilo katika Hifadhi ya Mikumi ambayo Agosti 7, mwaka huu ilifikisha miaka 60 tangu kuanzishwa.

Kama ambavyo ilitangazwa na viongozi wa Wekundu wa Msimbazi, mashabiki ilibidi waripoti saa 11:00 alfajiri  leo katika Stesheni ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) iliyopo Posta jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza safari saa 12:00 asubuhi kwa treni ya umeme maarufu SGR.

Licha ya muda huo wa kuripoti wapo ambao walifika mapema zaidi na wengine ilidaiwa walikesha hapo ili kupata nafasi ya kuwa sehemu ya tukio hilo ambalo lilielezwa kuwa ni bure kwa mabehewa matatu.

Ndani ya muda mfupi kulingana na idadi kubwa ya mashabiki waliojitikeza mabehewa hayo yalijaa mapema huku mashabiki wengine ikiwalazimu kukata tiketi kwa fedha  zao.

Uzinduzi huo ni kuelekea kwenye kilele cha tamasha la 16 la Simba Day ambapo huanza kwa wiki nzima wanachama na mashabiki wa timu hiyo katika matawi yote nchini kufanya kazi za kujitolea kwa jamii na kutoa misaada mbalimbali kwa wenye uhitaji.

Katika siku ya kilele mashabiki na wanachama hukusanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa tangu asubuhi ambako huwa na burudani mbalimbali zinazoongozwa na wasanii, muziki, ngoma na michezo mbalimbali ikiwamo kutambulishwa kwa kikosi kipya kabla ya kuhitimisha kuingia uwanjani kucheza mechi na mwaka huu itakipiga dhidi ya APR ya Rwanda

Kama wewe ni shabiki wa Simba na upo nyumbani, basi umepitwa na burudani za hapa na pale na hii ni kama sherehe kutokana na vaibu lililotawala katika kila behewa huku vigoma na vijembe vikitawala.

Mashabiki maarufu wa Wekundu wa Msimbazi wamekuwa vinara katika hilo, akiwemo Mwijaku ambaye ameonekana akitoa tambo mbalimbali tangu kuanza kwa safari hiyo.

Miongoni mwa nyimbo zilizonogesha safari hiyo umekuwa ukisikika ni ule wenye maneno maarufu kwa sasa ‘Ubaya Ubwela’

Related Posts